Matendo 8
8
1Naye Sauli alikua pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano.
Waumini wateswa na kutawanyika
Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya waumini wa Isa huko Yerusalemu, nao waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Yudea na Samaria. 2Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwomboleza sana. 3Lakini Sauli alianza kuangamiza kundi la waumini. Aliingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani.
Filipo ahubiri Injili huko Samaria
4Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipoenda. 5Filipo akaenda mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Al-Masihi#8:5 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.. 6Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza alizofanya, wakasikiliza kwa makini yale aliyosema. 7Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele, na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. 8Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.
Simoni mchawi
9Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, 10nao watu wote, wakubwa kwa wadogo, wakamsikiliza na kustaajabu, wakisema, “Mtu huyu ndiye ajulikanaye kama Uweza Mkuu wa Mungu.” 11Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake. 12Lakini watu walipomwamini Filipo akihubiri Injili ya ufalme wa Mungu na jina la Isa Al-Masihi, wakabatizwa, wanaume na wanawake. 13Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.
14Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko. 15Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu wa Mungu, 16kwa sababu Roho wa Mungu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Isa. 17Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho wa Mungu.
18Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho wa Mungu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha 19akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho wa Mungu.”
20Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! 21Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. 22Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Mwenyezi Mungu. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. 23Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”
24Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Mwenyezi Mungu, ili hayo mliyosema lolote lisinitokee.”
25Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana Isa, wakarudi Yerusalemu wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Samaria.
Filipo na towashi wa Kushi
26Basi malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara inayotoka Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.” 27Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa ameenda Yerusalemu ili kuabudu, 28naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi kwenye gari lake la vita akisoma kitabu cha nabii Isaya. 29Roho wa Mungu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”
30Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo unayoyasoma?”
31Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.
32Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko:
“Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni,
kama mwana-kondoo anyamazavyo
mbele yake yule amkataye manyoya,
hivyo hakufungua kinywa chake.
33Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake.
Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?
Kwa maana maisha yake yaliondolewa
kutoka duniani.”#8:33 Isaya 53:7, 8
34Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?” 35Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la Maandiko, akamweleza Injili ya Isa.
36Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?”
[ 37#8:37 Maandiko mengine ya kale hayana aya hii.Filipo akamwambia, “Ukiamini kwa moyo wako wote, unaweza kubatizwa.”
Akajibu, “Naamini kuwa Isa Al-Masihi ni Mwana wa Mungu.”] 38Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Filipo na yule towashi wakateremka kwenye maji pamoja, naye Filipo akambatiza. 39Nao walipotoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi. 40Filipo akajikuta Azoto; akasafiri akihubiri Injili katika miji yote hadi akafika Kaisaria.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.