Luka 11
11
Isa afundisha wanafunzi wake kuomba
(Mathayo 6:9-13)
1Siku moja, Isa alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana Isa, tufundishe kuomba, kama vile Yahya alivyowafundisha wanafunzi wake.”
2Akawaambia, “Mnapoomba, semeni:
“ ‘Baba yetu [uliye mbinguni]#11:2 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.,
jina lako litukuzwe,
ufalme wako uje. [
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.]#11:2 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.
3Utupatie kila siku riziki yetu.
4Utusamehe dhambi zetu,
kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.
Wala usitutie majaribuni
[bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu]#11:4 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya..’ ”
5Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu, 6kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa ale.’
7“Kisha yule aliye ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’ 8Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.
Omba, tafuta, bisha
(Mathayo 7:7-12)
9“Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 10Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
11“Je, kuna baba yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake? 12Au mtoto akimwomba yai atampa nge? 13Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wa Mungu wale wamwombao!”
Isa na Beelzebuli
(Mathayo 12:22-30; Marko 3:20-27)
14Basi Isa alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu wakashangaa. 15Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli#11:15 au Beelzebubu; pia 11:18, 19, yule mkuu wa pepo wachafu wote.” 16Wengine ili kumjaribu wakataka awaoneshe ishara kutoka mbinguni.
17Isa akajua mawazo yao, naye akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe itaanguka. 18Kama Shetani amegawanyika mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli. 19Kama mimi natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu nao je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 20Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umewajia.
21“Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama. 22Lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yeye humnyang’anya silaha zake zote alizozitegemea, na kuchukua nyara.
23“Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.
Mafundisho kuhusu pepo mchafu
(Mathayo 12:43-45)
24“Pepo mchafu anapomtoka mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ 25Naye anaporudi na kuikuta ile nyumba imefagiwa na kupangwa vizuri, 26ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”
27Ikawa Isa alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya umati ule wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”
28Isa akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”
Ishara ya Yona
(Mathayo 12:38-42)
29Umati wa watu walipokuwa wanazidi kuongezeka, Isa akaendelea kusema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona. 30Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. 31Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kuwahukumu watu wa kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Sulemani. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani. 32Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
Taa ya mwili
(Mathayo 5:15; 6:22-23)
33“Hakuna mtu yeyote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru. 34Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote pia umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote pia umejaa giza. 35Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyo ndani yako isiwe giza. 36Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yoyote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”
Isa awashutumu Mafarisayo na wataalamu wa Torati
(Mathayo 23:1-36; Marko 12:38-40)
37Isa alipomaliza kuzungumza, Farisayo#11:37 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. mmoja alimwalika nyumbani mwake kwa chakula. Isa akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani. 38Yule Farisayo akashangaa kwamba Isa hakunawa kwanza kabla ya kula.
39Ndipo Bwana Isa akamwambia, “Sasa, enyi Mafarisayo mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyang’anyi na uovu. 40Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye alitengeneza na ndani pia? 41Basi toeni sadaka ya vile mlivyo navyo, na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu.
42“Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kufanya haya ya pili bila kupuuza hayo ya kwanza.
43“Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kukalia viti vya mbele katika masinagogi#11:43 Nyumba za ibada na mafunzo., na kusalimiwa kwa heshima masokoni.
44“Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”
45Mtaalamu mmoja wa Torati akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.”
46Isa akamjibu, “Nanyi wataalamu wa Torati, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia.
47“Ole wenu, kwa sababu ninyi mnajenga makaburi ya manabii waliouawa na baba zenu. 48Hivyo ninyi mwashuhudia na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya. Wao waliwaua manabii, nanyi mnawajengea makaburi. 49Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’ 50Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, 51tangu damu ya Habili hadi damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote.
52“Ole wenu ninyi wataalamu wa Torati, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”
53Isa alipoondoka huko, walimu wa Torati na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali, 54wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.
Iliyochaguliwa sasa
Luka 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.