Yohana MT. 20
20
1HATTA siku ya kwanza ya sabato Mariamu Magdalene akaenda kaburini alfajiri, kungali giza bado, akaliona jiwe limeondolewa kaburini. 2Bassi akaenda mbio hatta kwa Simon Petro, na kwa mwanafunzi yule mwingine aliyependwa na Yesu, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. 3Bassi Petro akatoka, na mwanafunzi yule mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. 4Wakaenda mbio wawili pamoja: yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini; 5akainama, akaviona vitambaa vimewekwa; illakini hakuingia.
6Bassi akaja na Simon Petro, akimfuata, akaingia kaburini; akavitazama vitambaa vimewekwa, 7na ile leso iliyokuwa kichwani pake, haikuwekwa pamoja na vitambaa, bali imekunjwa, na kuwekwa mahali pa peke yake. 8Bassi ndipo akaingia nae mwanafunzi yule mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona, akaamini. 9Kwa maana hawajalifahamu andiko bado, kwamba imempasa kufufuka. 10Bassi wanafunzi wale wakaenda zao nyumbani kwao.
11Lakini Mariamu alikuwa amesimama karibu na kaburi, nje yake, analia; bassi, akilia hivi, akainama, akachungulia ndani ya kaburi; 12akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani, na mmoja miguuni, hapo ulipowekwa mwili wa Yesu. 13Nao wakamwambia, Bibi, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala sijui walikomweka. 14Alipokwisha kusema haya, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. 15Yesu akamwambia, Bibi, unalilia nini? Unamtafuta nani? Yeye, akidhani ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, kama umemchukua wewe, niambie ulipomweka, nami nitamwondoa. 16Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Rabboni (tafsiri yake Mwalimu). 17Yesu akamwambia, Usiniguse; kwa maana sijapaa kwa Baba yangu. Lakini enenda kwa ndugu zangu, ukawaambie, Ninapaa kwa Baba yangu na Baba yenu, kwa Mungu wangu na Mungu wenu. 18Mariamu Magdalene akaenda akawapasha wanafunzi khabari ya kwamba amemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia haya.
19Ikawa jioni katika siku ile ya kwanza ya sabato, na milango imefungwa walipokuwapo wanafunzi kwa khofu ya Wayahudi, akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani kwenu. 20Akiisha kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Bassi wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. 21Bassi Yesu akawaambia marra ya pili, Amani kwenu; kama Baba alivyonipeleka, nami nawatuma ninyi. 22Akiisha kusema haya, akawapulizia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. 23Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia, wamefungiwa.
24Tomaso, mmoja wa wathenashara aitwae Didumo, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. 25Bassi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika alama za misumari, na kutia mkono wangu uhavuni mwake, sitaamini kabisa. 26Baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo ndani marra ya pili, na Tomaso pamoja nao. Yesu akaja, milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani kwenu. 27Akiisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, ukatazame mikono yangu; kalete mkono wako, uutie katika ubavu wangu; wala nsiwe asiyeamini, bali aaminiye. 28Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu, na Mungu wangu. 29Yesu amwambia, Kwa kuwa umeniona, umeamini; wa kheri wasioona wakaamini. 30Bassi ziko ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki; 31lakini hizi zimeandikwa mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana MT. 20: SWZZB1921
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.