Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mose 24

24
Eliezeri anamposea Isaka mkewe Rebeka.
1Aburahamu alikuwa mkongwe mwenye siku nyingi, nyingi sana, naye Bwana alikuwa amembariki Aburahamu po pote.#1 Mose 12:2; Sh. 112:2-3. 2Ndipo, Aburahamu alipomwambia mtumishi wake aliyepata uzee nyumbani mwake, aliyezitunza mali zake zote: Uweke mkono wako chini ya kiuno changu,#1 Mose 47:29. 3nikuapishe kwake Bwana aliye Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi kwamba: Usimposee mwanangu mwanamke miongoni mwa wana wa kike wa Wakanaani, ambao ninakaa katikati yao!#1 Mose 28:1; 2 Mose 34:16. 4Ila uende katika nchi, nilikozaliwa, kwenye ndugu zangu kumposea mwanangu Isaka mkewe. 5Huyu mtumishi akajibu: Kama yule mwanamke hataki kunifuata kuja katika nchi hii, nimrudishe mwanao katika nchi ile, ulikotoka? 6Aburahamu akamwambia: Angalia sana, usimrudishe mwanangu kwenda huko! 7Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani mwa baba yangu na katika nchi, nilikozaliwa, aliniambia na kuniapia kwamba: Wa uzao wako ndio, nitakaowapa nchi hii. Yeye atatuma malaika wake, akutangulie, umpatie mwanangu mke huko.#1 Mose 12:1,7. 8Lakini yule mwanamke asipotaka kukufuata, basi, utakuwa umefunguliwa, nacho hiki kiapo, ninachokutakia, kitakuwa kimetanguka, lakini usimrudishe mwanangu kwenda huko! 9Ndipo, yule mtumishi alipouweka mkono wake chini ya kiuno cha bwana wake Aburahamu, akamwapia kufanya hivyo. 10Kisha yule mtumishi akachukua ngamia kumi za bwana wake kwenda safari, akachukua navyo vitu vizuri vyote vya bwana wake, kisha akaondoka, akaenda Mesopotamia kwenye mji wa Nahori.#1 Mose 11:31; 27:43. 11Huko nje ya mji kwenye kisima cha maji akawapumzisha ngamia; ikawa jioni, wanawake watokapo kuchota maji. 12Akaomba kwamba: Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, nipe kufanikiwa leo! Naye Bwana wangu Aburahamu mhurumie! 13Tazama, ninasimama hapa penye kisima cha maji, nao vijana wa kike wa watu wa humu mjini wanatoka kuchota maji. 14Nitakapomwambia kijana mmoja: Utue mtungi wako, ninywe! naye akisema: Haya! Unywe! Tena ngamia wako nao nitawanywesha, basi, awe yye, uliyemchagulia mtumishi wako Isaka! Nami ndipo, nitakapojua, ya kuwa umemhurumia bwana wangu.
15Alipokuwa hajaisha bado kuomba, mara akatokea Rebeka, binti Betueli aliyekuwa mwana wa Milka, mkewe Nahori, nduguye Aburahamu; naye alichukua mtungi begani.#1 Mose 22:23. 16Huyu kijana wa kike alikuwa mzuri sana wa kumtazama, tena alikuwa angali mwanamwali asiyejua mtu mume bado. Huyu akaja kushuka kisimani, napo alipokwisha kuujaza mtungi wake akapanda. 17Ndipo, yule mtumishi alipomkimbilia, akasema: Nipe maji kodogo ya mtungini mwako, ninywe! 18Naye akasema: Haya! Unywe, bwanangu! Akaushusha upesi mtungi wake mkononi mwake, akampa, anywe. 19Alipokwisha kumnywesha, akasema: Ngamia wako nao nitawachotea, hata wamalize kunywa. 20Akamwaga upesi maji ya mtungini ndani ya birika, akapiga mbio kwenda kisimani tena kuchota; ndivyo, alivyowachotea ngamia wake wote. 21Yule mtu akamstaajabu, lakini akanyamaza, apate kujua, kama Bwana amemtimizia vema safari yake, au kama sivyo. 22Ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtu akatoa pete la dhahabu lenye uzito kama wa shilingi na vikuku viwili vya dhahabu vyenye uzito wa sekeli kumi, ndio robo ya ratli, akamtia mikononi pake, 23akamwuliza: Wewe binti nani? Tena niambie, kama nyumbani mwa baba yako mna mahali pa kulala sisi. 24Akamwambia: Mimi ni binti Betueli, mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. 25Tena akamwambia: Majani ya kulisha ngamia kwetu ni mengi, hata mahali pa kulala usiku pako. 26Ndipo, yule mtu alipoinama na kumwangukia Bwana, 27akasema: Atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, kwa kuwa hakuzikomesha huruma zake na welekevu wake kwa Bwana wangu. Mimi nami Bwana ameniongoza njiani, akanifikisha nyumbani mwa ndugu zake.
28Lakini yule kijana alikuwa amekimbilia nyumbani mwa mama yake kuyasimulia maneno hayo yote. 29Naye huyo Rebeka alikuwa na kaka yake, jina lake Labani; huyu Labani akamkimbilia yule mtu huko nje kwenye kisima. 30Alipokuwa ameliona lile pete na vile vikuku mikononi pa dada, tena alipokuwa ameyasikia hayo maneno ya dada yake Rebeka kwamba: Haya ndiyo, yule mtu aliyoniambia, basi, hapo ndipo, alipomwendea yule mtu, akamkuta, akisimama kisimani na ngamia wake, 31akasema: Karibu, uliyebarikiwa na Bwana! Kwa nini unasimama nje? Mimi nimekutengenezea nyumba, hata mahali pa ngamia. 32Yule mtu alipoingia nyumbani, huyu akawafungua ngamia mizigo yao, akawapa mabua ya kulalia na majani ya kulisha, naye mwenyewe akampa maji ya kuiosha miguu yake nayo miguu ya watu waliokuwa naye. 33Alipoandaliwa vyakula yule akasema: Sitakula, mpaka niyaseme maneno yangu. Akamwambia: Yaseme!
34Akasema: Mimi ni mtumishi wake Aburahamu. 35Bwana amembariki sana bwana wangu, akawa mkubwa, akampa mbuzi na kondoo na ng'ombe na fedha na dhahabu na watumwa wa kiume na wa kike na ngamia na punda. 36Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume alipokwisha kuwa mzee; yeye ndiye, aliyempa yote, aliyo nayo. 37Kisha bwana wangu akaniapisha kwamba: Usimposee mwanangu mwanamke miongoni mwao wana wa kike wa Wakanaani, ambao ninakaa katika nchi yao! 38Ila uende nyumbani mwa baba yangu kwenye ndugu zangu kumposea mwanangu mkewe! 39Nilipomwambia bwana wangu: Labda yule mwanamke hatanifuata, 40ndipo, aliponiambia: Bwana, ambaye ninafanya mwenendo machoni pake, atatuma malaika wake kwenda na wewe, akupe, safari yako ifanikiwe, umposee mwanangu mke kwao ndugu zangu waliomo nyumbani mwa baba yangu.#1 Mose 17:1. 41Hapo utakapofika kwa ndugu zangu utakuwa uemfunguliwa, nacho kiapo, ninachokutakia, kitakuwa kimetanguka; usipompata kwao, utakuwa umefunguliwa kweli, nacho kiapo, ninachokutakia, kitakuwa kimetanguka kweli. 42Nilipofika leo hapo kisimani nikaomba kwamba: Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, afadhali nipe, hii safari yangu, niliyokuja huku, ifanikiwe! 43Tazama ninasimama hapa penye kisima cha maji! Itakuwa, kijana wa kike atoke kuchota maji, nami nitakapomwambia: Nipe maji kidogo ya mtungini mwako, ninywe! 44naye akiniambia: Haya! Unywe wewe mwenyewe! nao ngamia wako nitawachotea, basi, awe yeye mwanamke, Bwana aliyemchagulia mwana wa bwana wangu! 45Mimi nilipokuwa sijaisha bado kuyasema moyoni mwangu, mara nikamwona Rebeka, akitokea mwenye mtungi wake begani pake, akashuka kisimani kuchota. Ndipo, nilipomwambia: Nipe maji, ninywe! 46Naye akaushusha upesi mtungi wake toka begani, akasema: Haya! Unywe! Nao ngamia wako nitawapa, wanywe. Nilipokwisha kunywa, akawanywesha ngamia nao. 47Kisha nikamwuliza kwamba: Wewe binti nani? Akasema: Mimi binti Betueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia Nahori. Ndipo, nilipotia pete puani mwake na vikuku mikononi pake. 48Nikainama na kumwangukia Bwana, nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, kwa kuwa ameniongoza njiani kweli, nipate kumposea mwana wa bwana wangu binti ndugu yake. 49Sasa ninyi kama mkimpatia bwana wangu huruma na welekevu, niambieni! Kama sivyo, niambieni vile vile, nipate kugeuka na kujiendea kuumeni au kushotoni! 50Ndipo, Labani na Betueli walipojibu kwamba: Neno hili lmetoka kwake Bwana, sisi hatuwezi kukuambia neno baya wala jema. 51Tazama! Rebeka yuko mbele yako; mchukue kwenda naye, awe mkewe mwana wa bwana wako, kama Bwana alivyosema. 52Mtumishi wake Aburahamu alipoyasikia maneno yao akamwangukia Bwana hapo chini. 53Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na nguo, akampa Rebeka, naye umbu lake na mama yake akawapa matunzo. 54Wakala, wakanywa yeye nao wale watu waliokuwa naye, kisha wakalala.
Asubuhi walipoamka, akawaambia: Nipeni ruhusa kwenda kwa bwana wangu! 55Lakini kaka yake na mama yake wakasema: Acha kwanza, huyu kijana akae kwetu siku kidogo kama kumi! Halafu atakwenda, 56Naye akamwambia: Msinikawilishe! Kwani Bwana amenipa, safari yangu ifanikiwe, nipeni ruhusa, niende kwa bwana wangu! 57Ndipo, waliposema: Na tumwite huyu kijana, tumwulize, tuone, atakayoyasema! 58Wakamwita Rebeka, wakamwuliza: Unataka kwenda na mtu huyu! Akasema: Nitakwenda. 59Ndipo, walipompa ndugu yao Rebeka ruhusa kwenda pamoja na yaya wake na mtumishi wa Aburahamu na watu wake. 60Wakambariki Rebeka, wakamwambia: Ndugu yetu, na uwe mama ya maelfu na maelfu! Nao wa uzao wako na wayakalie malango ya adui zao!#1 Mose 22:17.
61Kisha Rebeka akaondoka na watumishi wake wa kike, wakipanda ngamia, wakamfuata yule mtu. Hivyo ndivyo, huyo mtumishi alivyomchukua Rebeka kwenda naye. 62Isaka alikuwa ametoka penye kisima cha Mwenye Uzima Anionaye, maana alikaa katika nchi ya kusini.#1 Mose 16:14; 25:11. 63Naye alikuwa ametoka kwenda shambani kuomba, jua lilipotaka kuchwa. Alipoyainua macho yake, mara akaona ngamia, wanaokuja. 64Rebeka naye akayainua macho yake; alipomwona Isaka akashuka upesi katika ngamia, 65akamwuliza yule mtumishi: Huyu mtu anayetujia hapa shambani ni nani? Yule mtumishi aliposema: Huyu ni bwana wangu, akachukua ukaya, akajifunika ushungi. 66Yule mtumishi akamsimulia Isaka mambo yote, aliyoyafanya. 67Ndipo, Isaka alipomwingiza Rebeka hemani mwa mama yake Sara, akamwoa, akawa mkewe, naye akampenda. Ndivyo Isaka alivyotulizwa moyo kwa ajili ya kufa kwa mama yake.#1 Mose 23:2.

Iliyochaguliwa sasa

1 Mose 24: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia