1 Mose 27
27
Yakobo anajipatia mbaraka ya Isaka kwa kumdanganya.
1Ikawa, Isaka alipokuwa mkongwe, macho yake yakatenda kiza, yasione; ndipo, alipomwita mwanawe mkubwa Esau, akamwambia: Mwanangu! Naye akamwitikia: Mimi hapa! 2Akasema: Tazama, nimekuwa mkongwe, siijui siku ya kufa kwangu. 3Sasa yachukue mata yako, ndio podo lako na upindi wako, uende porini kuniwindia nyama! 4Kisha unitengenezee kilaji cha urembo, kama ninavyokipenda, uniletee, nile, roho yangu ipate kukubariki, nikingali bado sijafa.#Ebr. 11:20.
5Lakini Rebeka alikuwa ameyasikia, Isaka aliyomwambia mwanawe Esau. Esau alipokwisha kwenda porini kuwinda nyama ya kumpelekea baba, 6Rebeka akamwambia mwanawe Yakobo kwamba: Tazama, nimesikia, baba yako akimwambia kaka yako Esau kwamba: 7Niletee nyama ya porini, unitengenezee kilaji cha urembo, nile, nipate kukubariki usoni pa Bwana kabla ya kufa kwangu! 8Sasa mwanangu, isikie sauti yangu, uyafanye nitakayokuagiza! 9Nenda makundini kunichukulia huko wana wawili wa mbuzi walio wazuri, nimtengenezee baba yako nyama zao kuwa kilaji cha urembo, kama anavyokipenda. 10Kisha utampelekea baba yako, ale, apate kukubariki kabla ya kufa kwake. 11Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka: Tazama, kaka yangu Esau ni mwenye manyoya, lakini mimi sinayo.#1 Mose 25:25. 12Labda baba atanipapasa; ndipo, nitakapokuwa kama mdanganyifu machoni pake; hivyo nitajipatia maapizo, sio mbaraka.
13Naye mama yake akamwambia: Maapizo yako na yanijie mimi, mwanangu! Isikie tu sauti yangu, uende kunichukulia wana wa mbuzi!
14Ndipo, alipokwenda, akawachukua, akamplekea mama yake, naye mama yake akawatengeneza kuwa kilaji cha urembo, kama baba yake alivyokipenda. 15Kisha Rebeka akazichukua nguo za mwanawe mkubwa Esau zilizo nzuri mno, alizokuwa nazo nyumbani mwake, akamvika mwanawe mdogo Yakobo. 16Nazo ngozi za wale wana wa mbuzi akamvika mikononi namo shingoni mlimokuwa hamna manyoya. 17Kisha akampa mwanawe Yakobo mkononi mwake hicho kilaji cha urembo pamoja na mkate, alioutengeneza nao.
18Alipoingia mwa baba yake akasema: Baba! Naye akasema: Mimi hapa! Wewe ndiwe nani, mwanangu? 19Yakobo akamwambia baba yake: Mimi ni Esau, mwanao wa kwanza; nimefanya, kama ulivyoniagiza. Inuka, ukae, ule nyama zangu, nilizokuwindia, roho yako ipate kunibariki! 20Isaka akamwuliza mwanawe: Mwanangu, umepataje nyama upesi hivyo? Akasema: Bwana Mungu wako amemtuma, anijie njiani. 21Kisha Isaka akamwambia Yakobo: Nikaribie, mwanangu, nikupapase, nione, kama wewe ndiwe mwanangu Esau, au kama siwe! 22Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, akampapasa, akasema: Sauti ni sauti yake Yakobo, lakini mikono ni mikono yake Esau. 23Hakumtambua, kwa kuwa mikono yake ilikuwa kama mikono ya kaka yake Esau yenye manyoya; ndipo, alipombariki. 24Alipomwuliza tena: Wewe ndie kweli mwanangu Esau? akasema: Ndio, ni mimi. 25Ndipo, alipomwambia: Niletee karibu, nile nyama, ulizoniwindia, mwanangu, roho yangu ipate kukubariki! Akazileta karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. 26Kisha baba yake Isaka akamwambia: Nikaribie, uninonee, mwanangu! 27Alipomkaribia na kumnonea, akausikia mnuko wa mavazi yake, akambariki akisema:
Tazama! Mnuko wa mwnangu
ni kama mnuko wa shamba, Bwana alilolibariki.
28Mungu akugawie umande wa mbinguni na manono ya nchi,
ngano zako ziwe nyingi, hata mvinyo vilevile!
29Makabila mazima na yakutumikie,
koo za watu zikuangukie!
Na uwe mkuu wa ndugu zako,
wana wa mama yako wakuangukie!
Atakayekuapiza na naapizwe!
Atakayekubariki na abarikiwe naye!#1 Mose 25:23; 12:3.
30Ikawa, Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokwisha kutoka usoni pa baba yake Isaka, ndipo, kaka yake Esau aliporudi kwa kuwinda. 31Naye akatengeneza kilaji cha urembo, akampelekea baba yake, akamwambia baba yake: Baba, inuka, ule nyama, mwanao alizokuwinda, roho yako ipate kunibariki! 32Ndipo, baba yake Isaka alipomwuliza: Wewe ndiwe nani? Akajibu: Mimi ni mwanao wa kwanza Esau. 33Ndipo, Isaka aliposhangaa mshangao mkubwa mno, akasema: Sasa ni nani yule mwinda nyama aliyeniletea nyama, nikala, ulipokuwa hujaja bado, nikambariki? Naye atakuwa amebarikiwa. 34Esau alipoyasikia haya maneno ya baba yake, akalia kilio kikubwa chenye uchungu mwingi sana, akamwambia baba yake: Baba, nibariki mimi nami!#Ebr. 12:17. 35Lakini akajibu: Ndugu yako mekuja kwa udanganyifu, akaipaat mbaraka yako. 36Akasema: Kumbe haitwi jina lake Yakobo (Mdanganyi)? Naye amenidanganya sasa mara mbili: Kwanza ameuchukua ukubwa wangu, sasa ameichukua mbaraka yangu nayo. Kisha akauliza: Hukuniwekea mbaraka nami?#1 Mose 25:26; 25:33. 37Isaka akajibu na kumwambia Esau: Tazama! Nimemweka kuwa mkubwa wako, nao ndugu zake wote nimempa, wamtumikie, hata ngano na mvinyo nimemfurikishia. Nawe wewe, mwanangu, nikufanyie nini? 38Ndipo, Esau alipomwuliza baba yake: Baba, unayo mbaraka moja tu? Baba, nibariki mimi nami! Kisha Esau akaipaza sauti yake, akalia. 39Ndipo, baba yake Isaka alipomwitikia na kumwambia:
Tazama! Hapo, utakapokaa,
manono ya nchi yatakuwa mbali,
nao umande wa mbinguni juu.
40Utajilisha mapato ya upanga wako,
utamtumikia ndugu yako;
lakini itakuwa, ukijikaza utalivunja kongwa,
litoke shingoni pako!#2 Fal. 8:20.
Esau anataka kumwua Yakobo.
41Esau akamchukua Yakobo kwa ajili ya hiyo mbaraka, baba yake aliyombariki; kwa hiyo Esau akasema moyoni mwake: Siku za kumwombolezea baba ziko karibu; zitakapopita, nitamwua ndugu yangu Yakobo. 42Rebeka alipopata habari ya lile shauri la mwananwe mkubwa Esau, akatuma kumwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia: Tazama! Kaka yako Esau anajituliza moyo kwa kwamba, akuue. 43Sasa mwnanangu, isikie sauti yangu! Inuka, ukimbilie Harani kwa kaka yangu Labani!#1 Mose 24:10. 44Na ukae kwake siku kidogo, mpaka machafuko ya kaka yako yatulie. 45Hapo, haya makali ya kaka yako yatakapotulia, aache kukuwazia mabaya kwa kuyasahau uliyomfanyizia, ndipo, nitakapotuma kukuchukua huko. Kwa nini mwataka, nifiwe nanyi wawili siku moja?
46Kisha Rebeka akamwambia Isaka: Ninachukizwa sana na kuwapo kwangu kwa ajili ya hao wanawake wa Kihiti. Kama Yakobo naye ataoa mwanamke miongoni mwao vijana wa kike wa Kihiti walio hivyo, kama hawa walivyo miongoni mwa vijana wa nchi hii, mimi nimeletewa nini huku?#1 Mose 26:34-35.
Iliyochaguliwa sasa
1 Mose 27: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.