1 Mose 28
28
Yakobo anakimbia kwwenda Harani.
1Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza kwamba: Usioe mwanamke katika vijana wa kike wa Kanaani!#1 Mose 24:3. 2Inuka, uende Mesopotamia nyumbani mwa Betueli, babake mama yako, umchukue mkeo huko katika wana wa kike wa Labani, umbu lake mama yako.#1 Mose 22:23; 24:29. 3Naye Mwenyezi Mungu akubariki, akupe kuzaa wana wengi sana, upate kuwa mkutano wa makabila ya watu! 4Akupe nayo mbaraka ya Aburahamu, wewe nao wa uzao wako wajao, upate kuichukua nchi hii ya ugeni wako, Mungu aliyompa Aburahamu.#1 Mose 12:2. 5Ndivyo, Isaka alivyomtuma Yakobo kwenda Mesopotamia kwa Mshami Labani, mwana wa Betueli, kaka yake Rebeka aliyekuwa mama yao Yakobo na Esau.
Ndoa ya pili ya Esau.
6Esau akaona, ya kuwa Isaka amembariki Yakobo na kumtuma kwenda Mesopotamia, achukue mke huko, tena ya kuwa hapo alipombariki amemwagiza kwamba: Usijichukulie mke katika vijana wa kike wa Kanaani! 7Tena akaona, ya kuwa Yakobo amemsikia baba yake na mama yake alipokwenda Mesopotamia. 8Tena Esau akaona, ya kama vijana wa kike wa Kanaani walikuwa wabaya machoni pa baba yake, Isaka. 9Ndipo, Esau alipokwenda kwa Isimaeli, akamchukua Mahalati, binti Isimaeli, mwana wa Aburahamu, umbu lake Nebayoti, kuwa mkewe pamoja na wakeze, aliokuwa nao.#1 Mose 26:34; 25:13.
Ndoto ya Yakobo: Ngazi ya kupandia mbinguni.
10Yakobo akaondoka Beri-Seba, akaenda Harani. 11Njiani alipofika mahali palipomfaa akalala hapo usiku, kwani jua lilikuwa limekuchwa. Akachukua jiwe la hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala mahali pale. 12Akaota, akaona ngazi, ilikuwa imesimikwa nchini, lakini ncha yake iligusa mbinguni; alipotazama akona, malaika wa Mungu wakipanda, tena wakishuka hapo.#Yoh. 1:51. 13Naye Bwana akamwona, akisimama juu, akasema: Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Aburahamu na Mungu wa Isaka. Nchi hii, unayoilalia, nitakupa wewe nao wa uzao wako.#1 Mose 12:7. 14Nao wa uzao wako watakuwa wengi kama mavumbi ya nchi hii, nawe utaenea upande wa baharini na upande wa maawioni kwa jua na upande wa kaskazini na upande wa kusini; namo mwako na katika uzao wako ndimo, koo zote za nchini zitakamobarikiwa.#1 Mose 12:3; 13:16; Gal. 3:16. 15Tazama! Niko pamoja na wewe, nikulinde po pote, utakapokwenda; nitakurudisha katika nchi hii, kwani sitakuacha, mpaka niyafanyize, niliyokuambia wewe. 16Yakobo alipoamka katika usingizi akasema: Kweli Bwana yuko mahali hapa, nami nilikuwa sikuyajua. 17Kwa hiyo akaogopa, akasema: Kumbe mahali hapa panaogopesha, hapa sipo pengine, ndipo Nyumba ya Mungu ilipo, ndipo lango la mbingu lilipo.#2 Mose 3:5.
Yakobo aliyoyaapa huko Beteli.
18Asubuhi na mapema Yakobo akaamka, akalichukua lile jiwe, aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kuwa kielekezo, akalimiminia mafuta juu yake, 19akapaita mahali pale jina lake Beteli (Nyumba ya Mungu), lakini kwanza ule mji uliitwa Luzi.#1 Mose 35:14-15. 20Kisha Yakobo akaapa kiapo kwamba: Mungu akiwa pamoja na mimi na kunilinda katika safari hii, ninayokwenda, akinipa vilaji vya kula na nguo za kuvaa, 21nipate kurudi na kutengemana nyumbani mwa baba yangu, Bwana atakuwa Mungu wangu, 22hata jiwe hili, nililolisimika kuwa kielekezo, litakuwa Nyumba ya Mungu, nayo yote, utakayonipa, nitakutolea fungu la kumi.#1 Mose 35:1,7.
Iliyochaguliwa sasa
1 Mose 28: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.