1 Mose 31
31
Yakobo anakimbia pamoja nao walio wake.
1Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani kwamba: Yakobo ameyachukua yote yaliyokuwa ya baba yetu; katika hayo yaliyokuwa yake baba yetu ndimo, alimoyatoa hayo mapato yake yote.#1 Mose 30:35. 2Ndipo, Yakobo alipoutazama uso wake Labani, akauona kuwa sio uleule, aliomwonyesha siku zote. 3Naye Bwana akamwabia Yakobo: Rudi katika nchi ya baba zako kwenye ndugu zako! Mimi nitakuwa pamona na wewe. 4Ndipo, Yakobo alipotuma kumwita Raheli naye Lea, waje porini kwake kwenye mbuzi na kondoo wake.#1 Mose 28:15. 5Akawaambia: Mimi nimeuona uso wa baba yenu kuwa sio, alionionyesha jana na juzi, lakini Mungu wa baba yangu alikuwa pamoja na mimi.#1 Mose 26:24. 6Nanyi mnajua, ya kuwa nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote. 7Lakini baba yenu amenidanganya na kuugeuza mshahara wangu mara kumi, lakini Mungu amemzuia, asiweze kunifanyizia kibaya. 8Aliposema: Wenye madoadoa watakuwa mshahara wako, mbuzi wote wakazaa wenye madoadoa; tena aliposema: Wenye vipakupaku watakuwa mshahara wako, mbuzi wote wakawa wenye vipakupaku.#1 Mose 30:32,39. 9Ndivyo, Mungu alivyoyachukua makundi ya baba yenu, akanipa mimi. 10Ikawa siku zile, mbuzi waliponyegeshwa, nikayainua macho yangu, nikatazama katika ndoto, nikaona, madume waliowapanda majike walikuwa wenye vipakupaku na wenye madoadoa na wenye marakaraka. 11Naye malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto: Yakobo! Nikasema: Mimi hapa! 12Akasema: Yainue macho yako, utazame, madume wote wanaowapanda majike ni wenye vipakupaku na wenye madoadoa na wenye marakaraka. Kwani nimeyaona yote, Labani aliyokufanyia. 13Mimi ni Mungu wa Beteli, ulikolipaka mafuta lile jiwe, ulilolisimika, na kuniapia kiapo. Sasa inuka, utoke katika nchi hii, urudi katika nchi hiyo, uliyozaliwa!#1 Mose 28:18-22. 14Ndipo, Raheli na Lea walipomjibu na kumwambia: Je? Sisi tuko na mafungu nyumbani mwa baba yetu, tutakayoyatwaa, yawe yetu sisi? 15Hatuwaziwi naye kuwa wageni, kwa kuwa ametuuza, akazila nazo zile fedha zetu?#1 Mose 29:18,27. 16Kwani mali hizo zote, Mungu alizozichukua kwa baba yetu, ni zetu sisi na za wana wetu; sasa yote, Mungu aliyokuambia, yafanye!
17Ndipo, Yakobo alipoondoka, nao wanawe na wake akawapandisha juu ya ngamia, 18akayachukua nayo makundi yake yote na mapato yake yote, aliyoyapata, nao nyama wengine waliokuwa mali zake, alizozipata kule Mesopotamia, aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani. 19Lakini Labani alikuwa amekwenda kuwakata kondoo wake manyoya. Kwa hiyo Raheli akapata kuviiba vinyago vya nyumbani vya baba yake. 20Ndivyo, Yakobo alivyomdanganya Mshami Labani, kwa kuwa hakumpasha habari, ya kama anataka kujiendea upesi hivi. 21Akatoroka yeye pamoja nayo yote yaliyokuwa yake, akalivuka lile jito na kuuelekeza uso wake kwenda mlimani kwa Gileadi.
Kupatana na kuagana na Labani.
22Siku ya tatu Labani akapashwa habari, ya kuwa Yakobo ametoroka. 23Ndipo, alipowachukua ndugu zake, akapiga mbio za kumfuata safari ya siku saba, akampata mlimani kwa Gileadi.#1 Mose 31:47. 24Lakini Mungu akamjia Mshami Labani katika ndoto usiku, akamwambia: Jiangalie, usiseme na Yakobo kwa ukali, ila kwa upole tu!#1 Mose 20:3; Fano. 16:7. 25Labani alimpofikia Yakobo karibu, Yakobo alikuwa amepiga hema lake mlimani, naye Labani na ndugu zake wakapanga mlimani kwa Gileadi. 26Labani akamwambia Yakobo: Umewezaje kuyafanya haya na kunidanganya, ukiwapeleka wanangu wa kike kama mateka wa upanga? 27Kwa nini umetoroka na kujifichaficha na kunidanganya, usiponipasha habari, nikapata kukusindikiza kwa furaha na kuimba na kupiga patu na mazeze? 28Wala hukunipatia kunoneana na wanangu wa kiume na wa kike. Kweli umefanya upumbavu. 29Ningependa, mkono wangu ungeweza kuwafanyizia mabaya, lakini Mungu wa baba yenu ameniambia usiku huu kwamba: Jiangalie, usiseme na Yakobo kwa ukali, ila kwa upole tu! 30Tena ulipokwenda safari yako kwa kuitunukia sana nyumba ya baba yako, kwa nini umekwiba miungu yangu? 31Yakobo akajibu na kumwambia Labani: Ni kwa kuwa nimeogopa na kusema moyoni, usininyang'anye wanao wa kike. 32Lakini utakayemwona, ya kuwa anayo miungu yako, na afe hapa mbele ya ndugu zetu! Jitafutie yaliyo yako kwangu, uyachukue! Naye Yakobo hakujua, ya kuwa Raheli ameiiba.#1 Mose 31:19. 33Labani alipoingia hemani mwa Yakobo namo hemani mwa Lea namo hemani mwa wale vijakazi wawili hakuona kitu. Alipotoka hemani mwa Lea akaingia hemanai mwa Raheli. 34Lakini Raheli alikuwa amevificha vinyago vya nyumbani ndani ya matandiko ya ngamia, akayakalia. Naye Labani alipoyapapasapapasa yote yaliyomo hemani hakuona kitu. 35Naye Raheli akamwambia baba yake: Usikasirike, bwana wangu! Kwani siwezi kuinuka mbele yako, kwani mambo yetu ya kike yamenipata. Kwa hiyo hakuviona vile vinyago vya nyumbani, ijapo alivitafuta po pote.
36Ndipo, Yakobo alipokasirika sana, akaanza kumgombeza Labani akianza kusema naye na kumwambia: Nimepotoa nini? Au nimekosa nini, ukijikaza kunifuata hivyo? 37Umevipapasapapasa vyombo vyangu vyote pia, lakini umeona kitu gani kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu walio na ndugu zako, watuamue sisi wawili. 38Sasa mimi nimekuwa miaka 20 kwako, majike wako wa kondoo na wa mbuzi hawakuharibu mimba, wala madume wako wa mbuzi na wa kondoo sikuwala. 39Walioraruliwa na nyama sikukupelekea, sikuwa na budi kuwalipa, ukawataka mikononi mwangu nao walioibiwa mchana, nao walioibiwa usiku.#2 Mose 22:12-13. 40Mambo yangu yamekuwa hivyo: mchana joto la jua limenichoma, usiku nao baridi ikafukuza usingizi, usiingie machoni pangu. 41Hivyo ndivyo, nilivyokutumikia nyumbani mwako miaka hii 20, miaka kumi na minne, niwapate hawa wano wawili wa kike, tena miaka sita, niyapate haya makundi yako, nawe umeugeuza mshahara wangu mara kumi.#1 Mose 29:20,30; 30:31-32. 42Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Aburahamu, Isaka anayemcha naye, asingalikuwa upande wangu, ungalinifukuza sasa mikono mitupu. Lakini Mungu ameuona ukiwa wangu na usumbufu wa mikono yangu, kwa hiyo amekata shauri usiku huu.#1 Mose 31:54.
43Labani akajibu na kumwambia Yakobo: Hawa wana wa kike ni wanangu, nao hawa wana ni wangu, nao hawa mbuzi na kondoo ni mbuzi na kondoo wangu, nayo yote, unayoyaona, ni yangu mimi. Basi, hawa wanangu wa kike nao hawa wana wao niwafanyie nini? 44Sasa njoo, tufanye agano mimi na wewe, lipate kutushuhudia mimi na wewe! 45Ndipo, Yakobo alipochukua jiwe, akalisimika kuwa kielekezo.#1 Mose 28:22. 46Kisha yakobo akawaambia ndugu zake, waokote mawe; ndipo, walipokwenda kuchukua mawe, wakayapanga kuwa chungu, kisha wakaja juu yake hilo chungu. 47Labani akaliita Yegari-Sahaduta (Chungu la Ushahidi), naye Yakobo akaliita Galeedi (Chungu Shahidi). 48Labani akasema; Chungu hili leo ni shahidi wetu mimi na wewe, kwa hiyo likaitwa Galeedi (Gileadi);#Yos. 22:27; 24:27. 49tena likaitwa Misipa (Chungulio), kwani alisema: Bwana na atuchungulie sisi, mimi na wewe, itakapokuwa, tusionane. 50Utakapowatesa hawa wanangu wa kike, au utakapochukua wake wengine kuliko hawa wanangu wa kike, kweli hakuna mtu shahidi huku kwetu sisi, lakini tazama, Mungu ni shahidi wetu sisi, mimi na wewe. 51Kisha Labani akamwambia Yakobo: Litazame chungu hili, litazame nalo hili jiwe, nililolisimika kuwa kielekezo chetu, mimi na wewe. 52Hili chungu na liwe shahidi, nacho hiki kielekezo kiwe ushuhuda wa kutukukataza, mimi nisilipite chungu hili kwenda kwako, wala wewe usilipite chungu hili kuja kwangu kufanya mabaya. 53Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Nahori aliye Mungu wa baba zao na atuamue! Ndipo, Yakobo alipoapa na kumtaja Mungu, baba yake Isaka aliyemcha.#1 Mose 16:5. 54Kisha Yakobo akachinja hapo mlimani ng'ombe ya tambiko, akawaalika ndugu zake kuja kula naye; walipokwisha kula wakalala usiku huko mlimani.#1 Mose 31:42.
55Kesho yake Labani akaamka na mapema, akanoneana na wanawe wa kiume na wa kike na kuwabariki; kisha Labani akaenda zake kurudi kwao.
Iliyochaguliwa sasa
1 Mose 31: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.