1 Mose 30
30
Wana wengine wa Yakobo.
1Raheli alipoona, ya kuwa hamzalii Yakobo wana, ndipo, alipomwonea dada yake wivu, akamwambia Yakobo: Unipatie wana! Nisipowapata nitakufa. 2Ndipo, makali ya Yakobo yalipomwakia Raheli, akamwambia: Je? Mimi ni kama Mungu aliyekunyima mazao ya tumbo?#Sh. 127:3. 3Akajibu: Tazama! Yuko kijakazi wangu Biliha, ingia kwake, azae magotini pangu, mimi nami nipate mlango kwake yeye.#1 Mose 16:2. 4Akampa kijakazi wake Biliha kuwa mkewe, naye Yakobo akaingia kwake. 5Hivyo Biliha akapata mimba, akamzalia Yakobo mtoto mume. 6Ndipo, Raheli aliposema: Mungu amenihukumia, akaisikia nayo sauti yangu, akanipa mtoto mume, kwa sababu hii akamwita jina lake Dani (Mhukumu). 7Kisha Biliha, kijakazi wake Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mtoto mume wa pili. 8Raheli akasema: Nimepiga vita vya Mungu vya kupigana na dada yangu, nami nikashinda. Kwa hiyo akamwita jina lake Nafutali (Vita vyangu).
9Lea alipoona, ya kuwa amekoma kuzaa, akamchukua kijakazi wake Zilpa, akampa Yakobo kuwa mkewe.#1 Mose 29:35. 10Huyu Zilpa, kijakazi wake Lea, akamzalia Yakobo mtoto mume; 11ndipo, Lea aliposema: Nina bahati, akamwita jina lake Gadi (Bahati). 12Zilpa, kijakazi wake Lea, akamzalia Yakobo mtoto mume wa pili; 13ndipo, aliposema: Mimi ni mwenye shangwe, kwani wanawake watanishangilia. Kwa hiyo akamwita jina lake Aseri (Shangwe).
14Rubeni alipotembea siku za mavuno ya ngano, akaona tunguja shambani akampelekea mama yake. Naye Raheli akamwambia Lea: Unigawie na mimi tunguja za mwanao! 15Lakini huyu akajibu: Haitoshi, ukimchukua mume wangu? Unazitakia nini hizi tunguja za mwanangu? Raheli akajibu: Basi, na alale kwako usiku huu, nipate tu tunguja za mwanao! 16Jioni Yakobo aliporudi toka shambani, Lea akamwendea njiani, akamwambia: Ingia kwangu! Kwani nimekununua leo kwa kutoa tunguja za mwanangu. Alipolala naye usiku huo, 17Mungu akamsikia Lea, akapata mimba, akamzalia Yakobo mtoto mume wa tano. 18Ndipo, Lea aliposema: Mungu amenipa mshahara wangu, kwa kuwa nimempa mume wangu kijakazi wangu, kwa hiyo akamwita jina lake Isakari (Mtu wa Mshahara). 19Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mtoto mume wa sita; 20ndipo, Lea aliposema: Mara hii Mungu amenipatia tunzo zuri. Sasa mume wangu atakaa kwangu, kwani nimemzalia watoto waume sita; kwa hiyo akamwita jina lake Zebuluni (Kao.) 21Baadaye akazaa mtoto mke, akamwita jina lake Dina.
22Ndipo, Mungu alipomkumbuka Raheli, Mungu akamsikia, akalifungua tumbo lake.#1 Sam. 1:19. 23Kwa hiyo naye akapata mimba, akazaa mtoto mume, akasema: Mungu ameniondolea yaliyonitia soni,#Yes. 4:1; Luk. 1:25. 24akamwita jina lake Yosefu (Huongeza) akisema: Bwana aniongezee mwana mwingine!
Werevu wa Yakobo wa kujipatia mali nyingi mno.
25Raheli alipokwisha kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani: Nipe ruhusa, niende kwetu katika nchi yangu! 26Nipe wake zangu na wanangu, ambao nilikutumikia, niwapate! Kisha niende zangu, kwani wewe unaujua utumishi wangu, niliokutumikia.#1 Mose 29:20,30. 27Naye Labani akamwambia: Ninataka kuona upendeleo machoni pako, kwa kuwa nimeona, ya kama Bwana amenibariki kwa ajili yako.#1 Mose 39:5. 28Akaendelea kusema: Ninakuomba, sema mshahara, unaotaka kwangu! Ndio, nitakaokupa. 29Akamwambia: Wewe unajua mwenyewe, jinsi nilivyokutumikia, tena jinsi makundi yako yalivyokua kwangu. 30Kwani kabla ya kuja kwangu yalikuwa madogo, lakini sasa yamesambaa kwa kuwa mengi, maana Bwana amekubariki pote, nilipokwenda. Sasa wao waliomo nyumbani mwangu niwafanyie kazi lini? 31Naye akamwuliza: Nikupe nini? Yakobo akamwambia: Usinipe cho chote! Nifanyie hili tu: acha, niwachunge tene mbuzi na kondoo wako na kuwaangalia! 32Tena nipite leo kwenye mbuzi na kondoo wako wote kuondoa kwao kondoo wote wenye mawaa na madoadoa nao wana weusi wote pia nao mbuzi wote wenye madoadoa na mawaa; basi, watakaozaliwa kuwa hivyo ndio mshahara wangu. 33Navyo ndiyo, nitakavyojulikana katika siku zijazo kuwa mwenye kweli: utakapokuja kuwatazama walio mshahara wangu, kila mbuzi asiye mwenye madoadoa na mawaa naye kila kondoo asiye mweusi atakuwa amekwibwa na mimi. 34Labani akamwitikia kwamba: Basi, na viwe hivyo, ulivyosema! 35Kisha Labani akaondoa siku hiyohiyo madume ya mbuzi wote waliokuwa wenye madoadoa na mawaa nao majike ya mbuzi wote waliokuwa wenye madoadoa na mawaa, wote pia waliokuwa wenye peupe, nao kondoo weusi wote, akawatia mikononi mwa wanawe, 36akawapeleka mwendo wa siku tatu, pawe hapo mahali pakubwa katikati yake yeye na Yakobo. Kisha Yakobo akapata kuwachunga mbuzi na kondoo wake Labani waliosalia.
37Kisha Yakobo akajitwalia matawi mabichi ya mikumbi na ya milozi na ya migude, akayabanduabandua, yapate mabaka meupe ya kutokeza sana huo weupe penye hayo matawi. 38Kisha akayasimika hayo matawi, aliyoyabandua hivyo, penye birika za kuwanyweshea maji mbuzi na kondoo kwamba: wao wakija kunywa maji, wayaone hayo, wanyegeshwe wakija kunywa. 39Nao mbuzi na kondoo waliponyegeshwa mbele ya hao matawi, ndipo, hao mbuzi na kondoo walipozaa wenye madoadoa na vipakupaku na mawaa. 40Hawa wana mbuzi Yakobo akawatenga, akawatanguliza mbele ya mbuzi na kondoo wengine, hao wote waliokuwa wake Labani wawatazame wale wenye madoadoa nao mbuzi na kondoo weusi; hivyo akajipatia makundi yake yeye, nayo haya hakuyachanganya nayo yake Labani. 41Kila mara mbuzi na kondoo wenye nguvu waliponyegeshwa, Yakobo akayaweka yale matawi machoni pao mbuzi na kondoo penye birika, wazidi kunyegeshwa wakiyaona hayo matawi. 42Lakini kwao wale mbuzi na kondoo waliokuwa wanyonge hakuyaweka; kwa sababu hii wale wanyonge wakawa wake Labani, lakini wale wenye nguvu wakawa wake Yakobo. 43Hivyo ndiyo, huyu mtu alivyopata mali nyingi sanasana, mbuzi na kondoo wake wakawa wengi, nao watumwa wa kiume na wa kike na ngamia na punda alikuwa nao.#1 Mose 12:16.
Iliyochaguliwa sasa
1 Mose 30: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.