1 Mose 42
42
Safari ya kwanza ya kaka zake Yosefu.
1Yakobo alipoona, ya kuwa Misri vyakula viko, Yakobo akawaambia wanawe: Mbona mnatazamiana? 2Akasema: Tazameni, nimesikia, ya kuwa Misri vyakula viko! Telemkeni kwenda huko, mtununulie ngano huko, tupate kupona, tusife! 3Basi, kaka zake Yosefu kumi wakatelemka kununua ngano kule Misri. 4Lakini Benyamini, nduguye Yosefu, Yakobo hakumtuma kwenda na kaka zake, kwani alisema: Labda ataona kibaya njiani. 5Wana wa Isiraeli wakaingia katikati yao wengine waliokwenda kununua ngano, kwani njaa ilikuwa imeingia hata katika nchi ya Kanaani.
6Naye Yosefu alikuwa mtawala nchi hiyo, naye ndiye aliyewauzia ngano watu wote wa nchi hiyo. Kaka zake Yosefu walipofika kwake wakamwinamia, mpaka nyuso zao zikifika chini. 7Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajitendekeza, kama hawajui, akasema nao maneno magumu, akawauliza: Mmetoka wapi? Wakasema: Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja huku kununua ngano. 8Ijapo Yosefu aliwatambua, wao hawakumtambua. 9Ndipo, Yosefu alipozikumbuka ndoto zake, alizoziota kwa ajili yao, kisha akawaambia: Mu wapelelezi, mmekuja kutazama, nchi hii inakokuwa wazi.#1 Mose 37:5-9. 10Wakamwambia: Sivyo, bwana wetu. Watumwa wako wamkuja tu kununua ngano. 11Sisi sote tu wana wa mtu mmoja, sisi tu watu wa kweli; watumwa wako hawajawa bado wapelelezi. 12Lakini akawaambia: Sivyo, mmekuja kutazama, nchi hii inakokuwa wazi. 13Ndipo, waliposema: Sisi watumwa wako tulikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na sasa mdogo wetu yuko kwa baba yetu, lakini mmoja hayupo. 14Lakini Yosefu akwaambia: Ni hivyo, nilivyowaambia kwamba: Mu wapelelezi. 15Kwa neno hili nitawajaribu: Hivyo, Farao alivyo mzima, hamtatoka huku, ndugu yenu mdogo asipokuja huku. 16Toeni mmoja miongoni mwenu, aende kumchukua ndugu yenu! Nanyi wengine mtafungwa. Hivyo mtaumbuliwa, kama maneno yenu ni ya kweli, au kama sivyo; hivyo, Farao alivyo mzima, mu wapelelezi. 17Kisha akawafunga kifungoni siku tatu.
18Siku ya tatu Yosefu akawaambia: Fanyeni hivi, mpate kupona! Kwani mimi ni mtu mwenye kumcha Mungu. 19Kama ninyi m watu wa kweli, mwenzenu mmoja tu afungwe kifungoni! Lakini ninyi wengine nendeni kupeleka ngano za kuondoa njaa nyumbani mwenu! 20Kisha sharti mniletee ndugu yenu mdogo, maneno yenu yajulike kuwa ya kweli, msife. Wakafanya hivyo. 21Ndipo, waliposemezana wao kwa wao: Kweli hapa tunalipishwa tuliyomkosea ndugu yetu. Tulipoona, roho yake ilivyosongeka, naye alipotulalamikia, hatukumsikia. Kwa sababu hii hangaiko hili limetupata.#Sh. 50:21. 22Rubeni akawajibu kwamba: Sikuwaambia ninyi kwamba: Msimkosee mtoto? Lakini mlikataa kunisikia; sasa mnaona, damu yake inalipizwa.#1 Mose 37:21-22. 23Nao hawakujua, ya kuwa Yosefu amewasikia, kwa kuwa walikuwa wanaye mkalimani. 24Ndipo, Yosefu alipoondoka kwenda kulia machozi. Aliporudi kusema nao, akamchukua Simeoni, akamfunga machoni pao.
25Kisha Yosefu akaagiza watu, wavijaze vyombo vyao ngano, nazo fedha zao za kila mmoja wazirudishe katika gunia lake, wawape hata pamba za njiani; nao wale wakawafanyizia hivyo. 26Kisha wakawachukuza punda wao mizigo yao ya ngano, wakatoka huko kwenda zao. 27Walipofika kambini, mmoja wao akalifungua gunia lake, ampe punda chakula, akaziona fedha zake hapo juu ndani ya gunia lake. 28Akawaambia ndugu zake: Kumbe fedha zangu zimerudishwa, zimo ndani ya gunia langu! Ndipo, mioyo yao ilipopigwa bumbuazi kwa kustuka, wakaambiana wao kwa wao: Mbona Mungu anatufanyizia haya?
Kaka zake Yosefu wanafika kwao.
29Waliporudi kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani wakamsimulia yote yaliyowapata njiani, wakasema: 30Yule bwana wa nchi hiyo ametuambia maneno magumu, akatusingizia kuwa watu wa kuipeleleza nchi hiyo, 31tukamwambia: Sisi tu watu wa kweli, hatujawa bado wapelelezi; 32sote tulikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu mmoja, naye mdogo sana yuko kwa baba yetu katika nchi ya Kanaani. 33Ndipo, yule bwana wa nchi hiyo alipotuambia: Hivi nitajua, ya kuwa m wakweli: mwenzenu mmoja mwacheni huku kwangu! Kisha chukueni vilaji vya kuondoa njaa nyumbani mwenu, mwende zenu! 34Kisha sharti mniletee ndugu yenu mdogo, nipate kujua, ya kuwa hamu wapelelezi, ya kuwa mu wakweli; ndipo, nitakapowapa naye ndugu yenu, nanyi mtaweza kuchuuza katika nchi hii. 35Ikawa walipoyamimina magunia yao wakaona kila mtu kifuko chake cha fedha katika gunia lake; walipoona, ya kuwa ni vifuko vya fedha zao kweli, wakashikwa na woga wote, wao na baba yao. 36Ndipo, baba yao Yakobo alipowaambia: Mwaninyang'anya wana wangu wote. Yosefu hayupo, Simeoni hayupo, sasa mnataka kumchukua Benyamini naye. Haya yote yamenipata! 37lakini Rubeni akamwambia baba yake: Wanangu wawili utawaua, nisipomrudisha Benyamini kwako. Mtie mkononi mwangu! Mimi nitamrudisha kwako. 38Lakini akasema: Huyu mwanangu hatatelemka pamoja nanyi, kwani kaka yake amekufa, naye amesalia peke yake; atakapopatwa na kibaya cho chote njiani katika hiyo safari mtakayokwenda mtanisukuma mimi mwenye mvi kushuka kuzimuni na kusikitika.#1 Mose 44:31.
Iliyochaguliwa sasa
1 Mose 42: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.