Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mose 41

41
Ndoto za Farao.
1Miaka miwili ilipopita, Farao akaota, akajiona, akisimama kando ya mto. 2Akaona, ng'ombe saba wazuri mno walionona wakitoka mtoni, wakapanda kwenda kula majanini. 3Kisha akaona, ng'ombe saba wengine wakitoka mtoni kuwafuata wale, ni wabaya mno wenye nyama kavu, wakaenda kusimama kando yao wale ng'ombe wa kwanza ukingoni kwa mto. 4Kisha hawa ng'ombe wabaya wenye nyama kavu wakawala wale ng'ombe saba wazuri walionona; ndipo, Farao alipoamka. 5Alipolala tena usingizi akaota mara ya pili, akaona, masuke saba yaliyo manene na mazuri yakitoka katika bua moja. 6Kisha akaona, masuke saba mengine yakichipuka nyuma yao, nayo ni membamba kwa kunyaushwa na upepo wenye joto. 7Haya masuke membamba yakayameza yale masuke manene yaliyojaa ngano. Ndipo, Farao alipoamka, akaona, ya kuwa ameota. 8Kulipokucha akahangaika rohoni, akatuma kuwaita waaguaji wote walioko Misri na wajuzi wote wa ndoto; lakini Farao alipowasimulia ndoto zake, hakupatikana aliyemfumbulia Farao maana ya hizo ndoto.#Dan. 2:2.
Yosefu anazifumbua ndoto za Farao.
9Ndipo, mkuu wa watunza vinywaji alipomwambia Farao kwamba: Leo hivi ninayakumbuka makosa yangu. 10Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinitia katika kifungo nyumbani mwake mkuu wao wanaomlinda mfalme, mimi pamoja na mkuu wa wachoma mikate; 11ndipo, tulipoota ndoto usiku mmoja mimi na yeye, tulikuwa tumeota kila mtu ndoto yake yenye maana yake yeye. 12Basi, mle tulikuwa na kijana wa Kiebureo, mtumwa wake mkuu wao wanaomlinda mfalme; tulipomsimulia ndoto zetu, akamfumbulia maana yao, kila mtu akamfumbuli ndoto yake yeye. 13Navyo, alivyotufumbulia, vikawa hivyo; mimi walinirudisha katika kazi, naye mwenzangu akanyongwa.
14Ndipo, Farao alipotuma kumwita Yosefu; wakamfungua upesi mle kifungoni, akajinyoa nywele, akavaa nguo nyingine, kisha akaja kuingia kwake mfalme. 15Farao akamwambia Yosefu: Nimeota ndoto, lakini hakuna anayezifumbua. Nimesikia habari yako kwamba: Unaposikia ndoto huifumbua. 16Yosefu akamjibu Farao kwamba: Sio mimi, Mungu na ayafunue yatakayompatia Farao utengemano!#1 Mose 40:8. 17Ndipo, Farao alipomwambia Yosefu: Katika ndoto yangu nimejiona, nikisimama ukingoni kwa mto. 18Mara nikaona, ng'ombe saba wazuri mno walionona wakitoka mtoni, wakapanda kwenda kula majanini. 19Kisha nikaona, ng'ombe saba wengine wakitoka mtoni kuwafuata wale, ni wenye kukonda kuwa wabaya sanasana kwa kuwa wenye nyama kavu; katika nchi zote za Misri sijaona bado ng'ombe wabaya kama hao. 20Hao ng'ombe wabaya waliokonda hivyo wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza walionona. 21Hao walipoingia tumboni mwao, haikujulikana, ya kuwa wamo tumboni mwao; nilipowatazama, walikuwa wabaya kama hapo kwanza. Ndipo, nilipoamka. 22Nilipoota tena nikaona, masuke saba yaliyojaa ngano kuwa mazuri yakitoka katika bua moja. 23Kisha nikaona masuke saba yaliyochipuka nyuma yao, nayo ni matupu na membamba kwa kunyaushwa na upepo wenye joto. 24Hayo masuke membamba yakayameza yale masuke mazuri. Nami nikawaambia waaguaji hizi ndoto, lakini hakuna anayeweza kuniambia maana.
25Ndipo, Yosefu alipomwmbia Farao: Ndoto za Farao ni moja; Mungu amemjulisha Farao atakayoyafanya. 26Ng'ombe saba wazuri ndio miaka saba, nayo masuke saba mazuri ndio miaka saba; ndoto hizi ni moja tu. 27Nao wale ng'ombe saba wenye kukonda vibaya waliotoka nyuma yao ndio miaka saba, nayo yale masuke saba matupu yaliyonyaushwa na upepo wenye joto ndio miaka saba ya njaa. 28Hili ndilo lile neno, nililomwambia Farao, ya kuwa Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya. 29Tazama! Inakuja miaka saba yenye shibe kubwa katika nchi nzima ya Misri. 30Baadaye itatokea miaka saba yenye njaa; ndipo, hiyo shibe yote itakaposahauliwa katika nchi ya Misri, nayo njaa itaimaliza nchi hii. 31Hiyo shibe haitajulikana kabisa katika nchi hii kwa ajili ya hiyo njaa itakayoifuata, kwani itakuwa nzito sana. 32Farao akiota mara mbili ndoto moja, ni kwamba: Shauri hili limekwisha kukatwa kwake Mungu, yeye Mungu atalifanya upesi. 33Sasa Farao na ajionee mtu mwenye akili na werevu wa kweli, amweke kuwa mkuu wa nchi ya Misri! 34Farao na ampe nguvu ya kuweka wasimamizi katika nchi hii, wawatoze watu wa Misri fungu la tano hiyo miaka saba ya shibe. 35Hivyo vyakula vyote na wavikusanye katika hiyo miaka saba mizuri ijayo, wazilimbike hizo ngano vyanjani mwa Farao, waziangalie vema kuwa akiba za kula wao waliomo mijini. 36Watu wa nchi hii na wawekewe hivyo vilaji, wapate kula, hiyo miaka saba ya njaa itakapoingia katika nchi ya Misri, watu wa nchi wasimalizike kwa njaa.
Yosefu anawekwa kuwa mkuu wa Misiri.
37Maneno haya yakawa mazuri machoni pake Farao napo machoni pao watumishi wake. 38Farao akawauliza watumishi wa: Je? Tutaona wapi mtu kama huyu mwenye roho ya Mungu?#Fano. 14:35. 39Kisha Farao akamwambia: Kuwa kuwa Mungu amekujulisha haya yote, basi, hakuna mwenye akili na werevu wa kweli kama wewe. 40Sasa wewe utakuwa mkuu wa nyumba yangu, nao watu wangu wote sharti wayafanye, kinywa chako kitakayowaambia; mimi tu nitakupita ukuu kwa kukikalia kiti cha ufalme.#Sh. 113:7; 37:37; Mbiu. 4:14. 41Farao akamwambia Yosefu tena: Tazama! Nimekupa ukuu wa nchi yote ya Misri nzima.#Tume. 7:10. 42Kisha Farao akaitoa pete yake kidoleni pake, akaitia katika kidole cha Yosefu, akamvika nguo nyeupe za bafta nzuri, akamtia mkufu wa dhahabu shingoni.#Est. 3:10; 8:2; Dan. 5:29. 43Kisha akamtembeza katika gari lake la kifalme la pili, akatanguliza watu waliopiga mbiu kwamba: Pigeni magoti! Ndivyo, alivyomweka kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. 44Kisha Farao akamwambia Yosefu: Kweli mimi ni Farao, lakini usipotaka wewe, mtu ye yote katika nchi yote ya Misri asiinue mkono wala mguu wake. 45Farao akamwita Yosefu Safenati-Panea (Mponya Wazima), akampa Asenati, binti Potifera, mtambikaji wa Oni, kuwa mkewe. Kisha Yosefu akatoka kwenda kuzitazama nchi zote za Misri. 46Hapo, Yosefu aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, alikuwa mwenye miaka 30, napo Yosefu alipotoka kwake Farao akatembea katika nchi zote za Misri.
Yosefu anaitunza vizuri nchi ya Misri.
47Hiyo miaka saba ya shibe nchi ikapata neema nyingi sana, 48naye Yosefu akavikusanya vilaji vyote vya hiyo miaka saba, iliyoipata nchi ya Misri, akavilimbika mijini akiagiza, vilaji vyote vya mashamba ya kila mji yaliyouzunguka yawekwe vyanjani mwake. 49Hivyo Yosefu akalimbika ngano, zikawa nyingi sana kama mchanga wa ufukoni, hata akaacha kuzipima, kwani hazikupimika. 50Mwaka wa njaa ulipokuwa haujaingia bado, Yosefu akazaliwa wana wawili, aliowazaa Asenati, binti Potifera, mtambikaji wa oni. 51Mwanawe wa kwanza Yosefu akamwita jina lake Manase (Msahaulishaji) kwa kwamba: Mungu amenisahaulisha masumbuko yangu yote nao mlango wote wa baba yangu. 52Naye wa pili akamwita jina lake Efuraimu (Mazao Mawili) kwa kwamba: Mungu amenipa kuzaa katika nchi ya ukiwa wangu.
53Hiyo miaka saba ya shibe, iliyoipata nchi ya Misri, ilipomalizika, 54ndipo, ile miaka saba ya njaa ilipoanza kuingia, kama Yosefu alivyosema; ikawa njaa katika nchi zote, ni nchi ya Misri tu iliyokuwa na chakula. 55Watu wote wa Misri walipoona njaa wakamililia Farao, awape chakula; naye Farao akawaambia watu wote: Nendeni kwa Yosefu! Nayo atakayowaambia yafanyizeni! 56Njaa ilipokwisha kuipata nchi yote nzima, ndipo, Yosefu alipovifungua vyanja vyote vya ngano vilivyokuwa kwao, akawauzia Wamisri ngano, nayo njaa ikawa kali katika nchi ya Misri. 57Watu wa nchi zote wakaja Misri kununua chakula kwa Yosefu, kwani njaa hiyo ilikuwa kali katika nchi zote.#1 Mose 12:10.

Iliyochaguliwa sasa

1 Mose 41: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia