Yohana 3
3
Nikodemo.
1*Kulikuwa na mtu wa Mafariseo, jina lake Nikodemo, aliyekuwa mkuu wa Wayuda.#Yoh. 7:50; 19:39. 2Huyo akamjia na usiku, akamwambia: Mfunzi mkuu, tunajua, ya kuwa wewe u mfunzi aliyetoka kwa Mungu, kwani hakuna mtu anayeweza kuvifanya vielekezo hivyo, unavyovifanya wewe, Mungu asipokuwa naye. 3Yesu akajibu, akamwambia: Kweli kweli nakuambia: Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.#1 Petr. 1:23. 4Nikodemo akamwambia: Mtu atawezaje kuzaliwa akiisha kuwa mzee? Ataweza kuingia tena tumboni mwa mama yake, apate kuzaliwa? 5Yesu akajibu: Kweli kweli nakuambia: Mtu asipozaliwa majini na Rohoni, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu;#Ez. 36:25-27; Mat. 3:11; Ef. 5:26; Tit. 3:5. 6kilichozaliwa na mwili ni mwili, nacho kilichozaliwa na Roho ni roho.#Yoh. 1:13; 1 Mose 5:3; Sh. 51:7; Rom. 8:5-9. 7Usistaajabu, nikikuambia: Sharti mzaliwe mara ya pili! 8Upepo huvuma, upendako, nawe huusikia uvumi wake, lakini hujui, uanziako wala ukomeako. Hivyo ndivyo, kila aliyezaliwa Rohoni alivyo. 9Nikodemo alipojibu na kumwuliza: Haya yawezekanaje kuwapo? 10Yesu akajibu, akamwambia: Je? Wewe u mfunzi wa Isiraeli, tena haya huyatambui? 11Kweli kweli nakuambia: Sisi huyasema, tuyajuayo; huyashuhudia, tuliyoyaona, lakini hamwupokei ushuhuda wetu!#Yoh. 7:16; 8:26,28. 12Msiponitegemea, nikiwaambia mambo ya ulimwenguni, mtanitegemeaje, nikiwaambia mambo ya mbinguni? 13Tena hakuna aliyepaa mbinguni, asipokuwa Mwana wa mtu aliyeshuka toka mbinguni.#Ef. 4:9. 14Kama Mose alivyokweza nyoka jangwani, vivyo hivyo hata Mwana wa mtu sharti akwezwe,#4 Mose 21:8-9. 15kila amtegemeaye apate uzima wa kale na kale.*
16*Kwani kwa hivyo, Mungu alivyoupenda ulimwengu, alimtoa Mwana wake wa pekee, kila amtegemeaye asiangamie, ila apate uzima wa kale na kale.#Rom. 5:8; 8:32; 1 Yoh. 4:9. 17Kwani Mungu hakumtuma Mwana wake ulimwenguni, auhukumu ulimwengu, ila ulimwengu upate kuokolewa naye.#Yoh. 12:47. 18Amtegemeaye hahukumiwi; asiyemtegemea amekwisha kuhukumiwa, kwani hakulitegemea Jina la Mwana wa Pekee wa Mungu#Yoh. 3:36; 5:24. 19Nayo hukumu ndiyo hii: mwanga ulikuja ulimwenguni, lakini watu waliipenda giza kuliko mwanga, kwa sababu matendo yao yalikuwa mabaya,#Yoh. 1:5,9-11. 20kwani kila mwenye kutenda maovu huuchukia mwanga, haji mwangani, matendo yake yasipatilizwe;#Ef. 5:13. 21lakini mwenye kuyafanya yaliyo ya kweli huja mwangani, matendo yake yaonekane, ya kuwa yametendeka katika Mungu.*
Yesu na Yohana.
22Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaenda katika nchi ya Yudea, akashinda kule pamoja nao akibatiza.#Yoh. 4:1-2. 23Lakini Yohana alikuwa akibatizia Enoni karibu ya Salemu, kwani kule kulikuwa na maji mengi, tena ndiko, watu walikomwendea, wakabatizwa naye, 24maana Yohana alikuwa hajatiwa bado kifungoni.#Mat. 14:3. 25Ikawa, wanafunzi wa Yohana walipobishana na Myuda kwa sababu ya maosho, 26wakaja kwa Yohana, wakamwambia: Mfunzi mkuu, aliyekuwa pamoja na wewe kule ng'ambo ya Yordani, yule uliyemshuhudia wewe, tazama, huyo anabatiza, watu wote wakimwendea.#Yoh. 1:26-34; 4:1-2. 27Yohana akajibu, akasema: Hakuna, mtu awezacho kukitwaa, asichopewa toka mbinguni.#Ebr. 5:4. 28Ninyi wenyewe mwanishuhudia, ya kuwa nalisema: Mimi siye Kristo ila nimetumwa, nimtangulie yeye.#Yoh. 1:20,23,27. 29Aliye mwenye mchumba ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama na kumsikiliza hufurahi sana kwa kuisikia sauti yake bwana arusi; basi, hiyo furaha yangu imetimia.#Mat. 9:15; 22:2. 30Yeye sharti akue, nami sharti nipunguke. 31Anayekuja toka juu ni mkuu kuliko wote; aliyetoka chini ni wa nchini, husema yaliyo ya nchini; anayekuja toka mbinguni ni mkuu kuliko wote.#Yoh. 8:23. 32Aliyoyaona nayo aliyoyasikia, ndiyo, anayoyashuhudia, lakini hakuna anayeupokea ushuhuda wake.#Yoh. 3:11. 33Aupokeaye ushuhuda wake huyu anamtambulisha Mungu waziwazi, kuwa ni wa kweli;#1 Yoh. 5:10. 34kwani aliyetumwa na Mungu huyasema maneno yake Mungu, naye Mungu haigawii Roho kwa kuipima.#Yoh. 1:33-34. 35Baba humpenda Mwana, akampa yote mkononi mwake.#Yoh. 5:20; Mat. 11:27. 36Amtegemeaye Mwana anao uzima wa kale na kale, lakini asiyemtii Mwana hataona uzima, ila makali ya Mungu humkalia.#Yoh. 3:18.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 3: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.