Yohana 4
4
Mwanamke Msamaria.
1Ilikuwa hapo, Bwana akitambua, ya kama Mafariseo wamesikia, ya kuwa Yesu anapata wanafunzi wengi, tena ya kuwa anabatiza kumpita Yohana,#Yoh. 3:22,26. 2ijapo Yesu mwenyewe hakubatiza mtu, ni wanafunzi wake tu. 3Ndipo, alipoondoka Yudea, akaenda kufika tena Galilea, 4lakini hakuwa na budi kushika njia ya kupita katikati ya Samaria.
5*Akafika penye mji wa Samaria, jina lake Sikari, ulio karibu ya kiunga, Yakobo alichompa mwanawe Yosefu;#1 Mose 48:22; Yos. 24:32. 6hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Kwa hivyo, Yesu alivyokuwa amechoka kwa mwendo, akakaa pale kisimani; ilikuwa kama saa sita. 7Alipokuja mwanamke Msamaria kuchota maji, Yesu akamwambia: Nipe, ninywe! 8kwani wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula. 9Ndipo, yule mwanamke Msamaria alipomwambia: Wewe uliye Myuda waniombaje ya kunywa mimi niliye mwanamke wa Kisamaria? Kwani Wayuda na Wasamaria huziana. 10Yesu akajibu, akamwambia: Kama ungekijua kipaji cha Mungu, tena kama ungemjua anayekuambia: Nipe, ninywe! wewe ungemwomba, naye angekupa maji yenye uzima.#Yoh. 7:38-39. 11Akamwambia: Bwana, hunacho cha kutekea, nacho kisima ni kirefu, basi, utayapata wapi hayo maji yenye uzima? 12Je? Wewe u mkubwa kuliko baba yetu Yakobo aliyetupa kisima hiki? Naye alikunywa humu mwenyewe na watoto wake na nyama wake wa kufuga. 13Yesu akajibu, akamwambia: Kila anayeyanywa maji haya ataona kiu tena;#Yoh. 6:58. 14lakini atakayeyanywa maji, nitakayompa mimi, hataona kiu kale na kale. Ila maji yale, nitakayompa, yatakuwa mwilini mwake chemchemi ya maji yabubujikayo, yamfikishe penye uzima wa kale na kale.*#Yoh. 6:27,35; 7:38-39. 15Yule mwanamke alipomwambia: Bwana, nipe maji hayo, nisipate kuona kiu tena, wala nisije hapa tena kuchota! 16akamwambia: Nenda, umwite mumeo! Kisha urudi hapa! 17Yule mwanamke alipojibu na kusema: Sina mume, Yesu akamwambia: Umesema kweli: Sina mume. 18Kwani waume watano ulikuwa nao, naye uliye naye sasa, siye mume wako; hili umesema kweli. 19Ndipo, yule mwanamke alipomwambia: Bwana, nakuona, ya kuwa wewe u mfumbuaji. 20Baba zetu walitambikia mlimani huku, nanyi husema: Yerusalemu ndipo, panapopasa kupatambikia.#5 Mose 12:5; Sh. 122.
21*Yesu akamwambia: Nitegemea mama, ya kuwa saa inakuja, itakapokuwa, msimtambikie Baba wala huku mlimani wala Yerusalemu! 22Ninyi hutambikia, msichokijua; sisi hutambikia, tunachokijua, kwani wokovu umeanzia kwa Wayuda.#2 Fal. 17:29-41; Yes. 2:3. 23Lakini saa inakuja, tena sasa iko, wenye kutambika kweli watakapomtambikia Baba kiroho na kikweli, kwani naye Baba huwataka wanaomtambikia hivyo. 24Mungu ni Roho, nao wanaomtambikia imewapasa kumtambikia kiroho na kikweli.*#2 Kor. 3:17. 25Ndipo, yule mwanamke alipomwambia: Najua, ya kuwa Masiya anakuja anayeitwa Kristo; yeye atakapokuja atatufunulia yote.#Yoh. 1:41. 26Yesu akamwambia: Mimi ndiye ninayesema nawe.#Yoh. 9:37.
27Hapo wanafunzi wake wakaja, wakashangaa, ya kuwa anasema na mwanamke; lakini hakuna aliyeuliza: Watafuta nini? au: Wasemaje naye? 28Lakini yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda mjini, akawaambia watu: 29Njoni, mtazame mtu aliyeniambia yote, niliyoyafanya, kama yeye siye Kristo! 30Ndipo, walipotoka mjini, wakamwendea.
31*Walipokuwa hawajafika, wanafunzi wakamhimiza wakisema: Mfunzi mkuu, ule! 32Alipowaambia: Mimi ninacho chakula, msichokijua ninyi,#Yoh. 4:34. 33wanafunzi wakasemezana: Yuko mtu aliyemletea chakula? 34Yesu akawaambia: Chakula changu ni kuyafanya, ayatakayo yeye aliyenituma, niimalize kazi yake.#Yoh. 17:4; Mat. 26:39. 35Ninyi hamsemi: Iko miezi minne bado, mavuno yatakapokuwapo? Tazameni, nawaambiani: Yainueni macho yenu, myatazame mashamba! Yamekwisha kuwa meupe, yavunwe.#Mat. 9:37; Luk. 10:2. 36Mvunaji hupokea mshahara, akakusanya vyakula, vimfikishe penye uzima wa kale na kale; hivyo mwishoni mpanzi hufurahi pamoja na mvunaji. 37Kwani hapo lile fumbo ni la kweli: Mwingine hupanda, mwingine huvuna. 38Mimi naliwatuma, mvune, msiyoyafanyia kazi; wengine wamefanya kazi, ninyi mkaingia kazini mwao.
39Kisha Wasamaria wengi wa mji ule wakamtegemea kwa ajili ya neno, yule mwanamke alilomshuhudia kwamba: Ameniambia yote, niliyoyafanya. 40Kwa hiyo Wasamaria walipomjia wakamtaka, akae kwao. Akakaa huko siku mbili. 41Kisha waliomtegemea kwa ajili ya neno lake mwenyewe wakawa wengi sana, 42wakamwambia yule mwanamke: Hatumtegemei tena kwa vile, ulivyotuambia, kwani wenyewe tumemsikia, tukamjua: Ni kweli, huyu ndiye mwokozi wa ulimwengu.*
43Siku mbili zilipopita, akatoka huko kwenda Galilea.#Mat. 4:12. 44Kwani Yesu mwenyewe alishuhudia, ya kuwa mfumbuaji haheshimiwi kwao, mwenyewe alikokulia.#Mat. 13:57; Mar. 6:4; Luk. 4:24. 45Alipofika Galilea, Wagalilea wakampokea, kwani walikuwa wameyaona yote, aliyoyatenda Yerusalemu siku za sikukuu; kwani nao walikuwa wamekwenda kule siku za sikukuu.#Yoh. 2:23.
Mwana wa mtu wa kifalme.
46Akafika tena Kana wa Galilea, alikogeuza maji kuwa mvinyo.#Yoh. 2:1,9.
*Kulikuwa na mtu wa kifalme aliyeuguliwa na mwana wake huko Kapernaumu. 47Huyo aliposikia, ya kuwa Yesu ametoka Yudea, akafika Galilea, akaondoka, akamwendea, akambembeleza, ashuke, amponye mwanawe, kwani alitaka kufa. 48Lakini Yesu akamwambia: Msipoona vielekezo na vioja hamnitegemei.#Yoh. 2:18; 1 Kor. 1:22. 49Yule mtu wa kifalme alipomwambia: Bwana, shuka, mtoto wangu asije kufa! 50Yesu akamwambia: Jiendee, mwana wako yuko mzima! Yule mtu akalitegemea neno, Yesu alilomwambia, akaenda zake. 51Angali akishuka, watumwa wake wakaja kukutana naye wakisema: Mtoto wako yuko mzima! 52Akawauliza saa, alipoanzia kuwa hajambo kidogo. Walipomwambia: Jana saa saba joto limemtoka, 53baba akatambua, ya kuwa ni saa ileile, Yesu alipomwambia: Mwana wako yuko mzima. Ndipo, yeye nao waliokuwamo mwake walipomtegemea wote. 54Hiki ndicho kielekezo cha pili, Yesu alichokifanya alipotoka Yudea kwenda Galilea.*#Yoh. 2:11,23.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 4: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.