Yohana 5
5
Mgonjwa ziwani pa Betesida.
1*Kisha ilipokuwa sikukuu ya Wayuda, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. 2Kule Yerusalemu karibu ya Lango la Kondoo kulikuwako kiziwa kiitwacho Kiebureo Betesida; hapo palikuwa na vibanda vitano. 3Humo mlikuwa na wagonjwa wengi, kama vipofu na viwete na wenye kupooza; wote walilala mle wakingoja, maji yatukuswe. 4Kwani mara kwa mara palishuka malaika kiziwani, akayatikisa maji; hapo, maji yalipoisha kutikiswa, aliyeingia wa kwanza akapona ugonjwa wo wote uliomshika. 5Pale palikuwa na mtu aliyekuwa hawezi miaka 38. 6Yesu alipomwona huyo, anavyolala, akatambua, ya kuwa imemwishia hapo miaka mingi, akamwambia: Unataka kuwa mzima? 7Mgonjwa akamjibu: Bwana, sina mtu wa kunitia kiziwani, maji yanapotikiswa. Kila mara mimi ninapokwenda, mwingine hushuka mbele yangu. 8Yesu akamwambia: Inuka, jitwishe kitanda chako, upate kwenda zako!#Mat. 9:6. 9Papo hapo yule mtu akawa mzima, akajitwisha kitanda chake, akaenda zake.#Yoh. 9:14.
10Lakini siku ile ilikuwa ya mapumziko. Kwa hiyo Wayuda walimwambia yule aliyeponywa: Leo ni siku ya mapumziko, huna ruhusa ya kukichukua kitanda.#Yer. 17:21-22. 11Lakini akawajibu: Yule aliyenipa kuwa mzima ameniambia: Jitwishe kitanda chako, upate kwenda zako! 12Wakamwuliza: Nani huyo mtu aliyekuambia: Jitwishe, upate kwenda zako? 13Lakini yule aliyeponywa hakumjua. Kwani Yesu alikuwa amepaepuka, kwa sababu hapo palikuwa na kundi la watu wengi. 14Kisha Yesu akamwona Patakatifu, akamwambia: Tazama, umepata kuwa mzima! Usikose tena, maana lisikujie jambo lililo baya kuliko lile!* 15Ndipo, yule mtu alipoondoka, akawaambia Wayuda: Ni Yesu aliyenipa kuwa mzima. 16Kwa hiyo Wayuda wakamnyatia Yesu, kwa sababu alivifanyia hivyo siku ya mapumziko.#Mat. 12:14. 17Lakini Yesu akawajibu: Baba yangu hufanya kazi mpaka sasa, nami naifanya.#Yoh. 9:4. 18Kwa hiyo Wayuda walikaza kutafuta njia ya kumwua, kwani hakuvunja mwiko tu wa siku ya mapumziko, ila Mungu naye alimwita Baba yake akijilinganisha na Mungu.#Yoh. 7:30; 10:33.
19*Yesu akajibu, akawaambia: Kweli kweli nawaambiani: Hakuna, Mwana awezacho kukifanya kwa nguvu yake, asipokuwa amemwona Baba, anavyokifanya. Kwani yule anavyovifanya, hivyo naye Mwana huvifanya vile vile.#Yoh. 3:11,32. 20Kwani Baba anampenda Mwana, akamwonyesha vyote, anavyovifanya. Nayo matendo yaliyo makubwa kuliko haya atamwonyesha, ninyi mpate kushangaa.#Yoh. 3:35. 21Kwani Baba, anavyowaamsha wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima, anaowataka. 22Kwani hata kuhukumu Baba hamhukumu mtu, ila hukumu yote amempa Mwana,#Dan. 7:13-14; Tume. 17:31. 23wote wapate kumheshimu Mwana, kama wanavyomheshimu Baba. Mtu asiyemheshimu Mwana hamheshimu naye Baba aliyemtuma.#Fil. 2:10-11; 1 Yoh. 2:23. 24Kweli kweli nawaambiani: Mtu anayelisikia neno langu na kumtegemea aliyenituma anao uzima wa kale na kale, hafiki penye hukumu, ila ametoka penye kufa na kuingia penye uzima.#Yoh. 3:16,18. 25Kweli kweli nawaambiani: Saa inakuja na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti yake Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watapata kuwa wazima.#Ef. 2:5-6. 26Kwani kama Baba alivyo Mwenye uzima, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa Mwenye uzima naye.#Yoh. 1:1-4; 10:18. 27Akampa nao uwezo wa kuhukumu, kwani ndiye Mwana wa mtu.#Yoh. 5:22; Dan. 7:13-14. 28Msilistaajabu hilo la kwamba: Saa inakuja, ndipo, wote waliomo makaburini watakapoisikia sauti yake. 29Nao walioyafanya mema watatoka na kufufukia uzima, nao walioyafanya maovu watatoka na kufufukia hukumu.*#Yoh. 6:40; Dan. 12:2; Mat. 25:46; 2 Kor. 5:10. 30Mimi siwezi kufanya cho chote kwa shauri langu; nahukumu, kama ninavyosikia; nayo hukumu yangu huwa yenye wongofu, kwani siyatafuti, niyatakayo mimi, ila yeye aliyenituma ayatakayo.#Yoh. 5:19; 6:38.
31Mimi ninapojishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu sio wa kweli. 32Yuko mwingine anayenishuhudia, nami naujua ushuhuda wake, alionishuhudia, ya kuwa ndio wa kweli.#Yoh. 5:36-37. 33Ninyi mlituma kwa Yohana, naye akayashuhudia yaliyo ya kweli.#Yoh. 1:19-34. 34Lakini mimi sitaki, mtu anishuhudie, ila nayasema haya, ninyi mpate kuokoka. 35Yule alikuwa taa inayowaka na kuangaza; lakini ninyi mlitaka kushangilia kitambo penye mwanga wake. 36Lakini mimi ninao ushuhuda ulio mkubwa kuliko wa Yohana. Kwani zile kazi, Baba alizonipa, nizimalize, kazi zizo hizo, ninazozifanya, hunishuhudia, ya kuwa Baba amenituma.#Yoh. 1:33; 3:2; 1 Yoh. 5:9. 37Naye Baba aliyenituma yeye amenishuhudia. Ninyi hamjaisikia bado sauti yake, wala hamjaiona sura yake,#Mat. 3:17. 38wala Neno lake hamnalo mioyoni mwenu, likae humo. Kwani yule, aliyemtuma, ndiye, ninyi msiyemtegemea.
39*Chunguzeni katika Maandiko! Kwani ninyi hudhani: Humo ndimo, mtakamopatia uzima wa kale na kale. Nayo ndiyo kweli yanayonishuhudia.#Luk. 24:27,44; 2 Tim. 3:15-17. 40Lakini ninyi hamtaki kuja kwangu, mpate uzima. 41Mimi sitaki kutukuzwa na watu. 42Lakini nimewatambua ninyi, ya kuwa hamnao upendo wa Mungu mioyoni mwenu. 43Mimi nimekuja kwa Jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei. Mwingine atakapokuja kwa jina lake mwenyewe, huyo ndiye, mtakayempokea.#Mat. 24:5. 44Mwawezaje kunitegemea ninyi mnaotukuzana? Lakini utukufu utokao kwake Mungu wa pekee hamwutafuti.#Yoh. 12:42-43; 1 Tes. 2:6. 45Msiniwazie ya kwamba: Mimi nitawasuta kwa Baba; yuko msutaji wenu, ndiye Mose, ninyi mliyemngojea.#5 Mose 31:26-27. 46Kwani kama mngemtegemea Mose, basi, mngenitegemea nami, kwani yeye aliandika mambo yangu mimi.#1 Mose 3:15; 49:10; 5 Mose 18:15. 47Lakini msipoyategemea, aliyoyaandika yeye, mtayategemeaje, ninayoyasema mimi?*#Luk. 16:31.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 5: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.