Yohana 14
14
Isa awatia moyo wanafunzi wake
1Isa akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mnamwamini Mungu, mniamini pia. 2Nyumbani mwa Baba#14:2 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningewaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo nanyi mpate kuwepo. 4Ninyi mnajua njia ya kufika ninakoenda.”
Isa ndiye njia ya kwenda kwa Baba
5Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakoenda, tutaijuaje njia?”
6Isa akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kupitia kwangu. 7Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”
8Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, na hiyo itatutosha.”
9Isa akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuoneshe Baba’? 10Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba, na Baba yuko ndani yangu; la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. 12Amin, amin nawaambia, yeyote anayeniamini mimi, kazi ninazozifanya naye atazifanya. Naam, na atazifanya kazi kubwa kuliko hizi, kwa sababu mimi ninaenda kwa Baba. 13Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14Mkiniomba lolote kwa Jina langu, nitalifanya.
Isa aahidi Roho wa Mungu
15“Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi, naye anakaa ndani yenu. 18Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja kwenu. 19Bado kitambo kidogo na ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona. Kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. 20Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, na ninyi mko ndani yangu, na mimi niko ndani yenu. 21Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
22Ndipo Yuda (siyo Iskariote) akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”
23Isa akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu, na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.
25“Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26Lakini huyo Msaidizi, yaani huyo Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27Amani nawaachia; amani yangu nawapa. Amani hii ninayowapa si kama ile ulimwengu unatoa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
28“Mlisikia nikisema, ‘Ninaenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngenipenda, mngefurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi. 29Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru.
“Haya inukeni; twendeni zetu.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 14: ONMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.