Mwanzo 11:1-9
Mwanzo 11:1-9 BHN
Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale. Basi, ikawa watu waliposafirisafiri kutoka mashariki, walifika katika nchi tambarare huko Shinari, wakakaa. Kisha wakaambiana, “Haya! Na tufyatue matofali, tuyachome moto vizuri.” Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, “Na tujijengee mji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.” Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu. Mwenyezi-Mungu akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa. Haya, na tushuke chini na kuivuruga lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.” Hivyo, Mwenyezi-Mungu akawatawanya mahali pote duniani, nao wakaacha kuujenga ule mji. Mji huo ukaitwa Babeli, kwa sababu huko ndiko Mwenyezi-Mungu alikoivuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko akawatawanya watu kila mahali duniani.