Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 52

52
Mungu ataikomboa Yerusalemu
1 #52:1 Taz Ufu 21:2,27 Amka! Amka!
Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni!
Jivike mavazi yako mazuri,
ewe Yerusalemu, mji mtakatifu.
Maana hawataingia tena kwako
watu wasiotahiriwa na walio najisi.
2Jikungute mavumbi, uinuke
ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara!
Jifungue minyororo yako shingoni,
ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka.
3Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja. 4Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote. 5#52:5 Taz Rom 2:24 Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku. 6Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!”
7 #52:7 Taz Nah 1:15; Rom 10:15; Efe 6:15 Tazama inavyopendeza
kumwona mjumbe akitokea mlimani,
ambaye anatangaza amani,
ambaye analeta habari njema,
na kutangaza ukombozi!
Anauambia mji wa Siyoni:
“Mungu wako anatawala!”
8Sikiliza sauti ya walinzi wako;
wanaimba pamoja kwa furaha,
maana wanaona kwa macho yao wenyewe,
kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni.
9Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu!
Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake,
ameukomboa mji wa Yerusalemu.
10Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu,
mbele ya mataifa yote.
Atawaokoa watu wake,
na ulimwengu wote utashuhudia.
11 #52:11 Taz 2Kor 6:17 Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa;
msiguse kitu chochote najisi!
Ondokeni huku Babuloni!
Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu.
12Safari hii hamtatoka kwa haraka,
wala hamtaondoka mbiombio!
Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni,
Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma.
Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu
13Mungu asema hivi:
“Mtumishi wangu atafanikiwa;
atatukuzwa na kupewa cheo,
atapata heshima kuu.
14Wengi waliomwona walishtuka,
kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa;
hakuwa tena na umbo la kibinadamu!
15 #52:15 Taz Rom 15:21 Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi.
Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake,
maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa,
na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 52: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia