Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 53

53
1 #53:1 Taz Yoh 12:38; Rom 10:16 Nani aliyeamini mambo tuliyosikia?
Nani aliyetambua kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu ulihusika?
2Maana, mbele yake Mwenyezi-Mungu,
mtumishi wake alikua kama mti mchanga,
kama mzizi katika nchi kavu.
Hakuwa na umbo wala sura ya kutupendeza,
wala hakuwa na uzuri wowote wa kutuvutia.
3Alidharauliwa na kukataliwa na watu,
alikuwa mtu wa uchungu na huzuni.
Alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu;
alidharauliwa na tukamwona si kitu.
4 #53:4 Taz Mat 8:17 Hata hivyo alivumilia majonzi yetu,
na kubeba huzuni zetu.
Sisi tulifikiri amepata adhabu,
amepigwa na Mungu na kuteswa.
5 #53:5 Taz 1Pet 2:24 Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu,
aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu.
Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai;
kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6 #53:6 Taz 1Pet 2:25 Sisi sote tumepotea kama kondoo,
kila mmoja wetu ameelekea njia yake.
Lakini Mwenyezi-Mungu alimtwika adhabu,
ambayo sisi wenyewe tuliistahili.
7 #53:7 Taz Ufu 5:6 Alidhulumiwa na kuteswa,
lakini alivumilia kwa unyenyekevu,
bila kutoa sauti hata kidogo.
Alikuwa kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni,
kama kondoo akaavyo kimya anapokatwa manyoya.
Hakutoa sauti hata kidogo. #53:7-8 Taz Mate 8:32-33
8Alidhulumiwa, akahukumiwa na kupelekwa kuuawa;
na hakuna mtu aliyejali yanayompata.
Alifukuzwa kutoka nchi ya walio hai,
kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9 #53:9 Taz 1Pet 2:22 Walimzika pamoja na wahalifu;
katika kifo aliwekwa pamoja na matajiri,
ingawa hakutenda ukatili wowote,
wala hakusema neno lolote la udanganyifu.
10Mwenyezi-Mungu alipenda kumwumiza
na kumweka katika huzuni.
Alijitoa mhanga kwa ajili ya kuondoa dhambi.
Mtumishi wa Mungu atakuwa na wazawa;
ataishi maisha marefu.
Yeye ndiye atakayetimiza mpango wa Mwenyezi-Mungu.
11Mungu asema:
“Baada ya kutaabika sana,
mtumishi wangu atafurahi.
Kwa kuwajibika kwake kikamilifu,
atatosheka na matokeo hayo.
Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwadilifu
atawafanya wengi wawe waadilifu
Yeye atazibeba dhambi zao.#53:11 atazibeba dhambi zao: Yaani kwa mateso yake adhabu ya dhambi ambayo watu walistahili imempata yeye nao watu wakasamehewa.
12Kwa hiyo, nitamweka katika cheo cha wakuu,
atagawa nyara pamoja na wenye nguvu;
kwa kuwa alijitolea mwenyewe kufa,
akawekwa katika kundi moja na wakosefu,
alizibeba dhambi za watu wengi,
akawaombea msamaha hao wakosefu.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 53: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia