Maombolezo 4:12-22
Maombolezo 4:12-22 BHN
Wafalme duniani hawakuamini wala wakazi wowote wa ulimwenguni, kwamba mvamizi au adui angeweza kuingia malango ya Yerusalemu. Hayo yalisababishwa na dhambi za manabii wake, yalitukia kwa sababu ya uovu wa makuhani wake ambao walimwaga damu ya waadilifu mjini kwake. Walitangatanga barabarani kama vipofu, walikuwa wamekuwa najisi kwa damu, hata asiwepo mtu yeyote wa kuwagusa. Watu waliwapigia kelele wakisema: “Tokeni, nendeni zenu enyi mlio najisi! Tokeni, tokeni, msiguse chochote.” Hivyo wakawa wakimbizi na kutangatanga; watu wa mataifa walitamka: “Hawa hawatakaribishwa kukaa kwetu!” Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwatawanya, wala hatawajali tena. Makuhani hawatapata tena heshima, wazee hawatapendelewa tena. Tulichoka kukaa macho kungojea msaada; tulikesha na kungojea kwa hamu taifa ambalo halikuweza kutuokoa. Watu walifuatilia hatua zetu, tukashindwa kupita katika barabara zetu. Siku zetu zikawa zimetimia; mwisho wetu ukawa umefika. Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai, walitukimbiza milimani, walituvizia huko nyikani. Walimnasa yule ambaye maisha yetu yalimtegemea, yule mfalme aliyewekwa wakfu wa Mwenyezi-Mungu, yule ambaye tulisema: “Chini ya ulinzi wake tutaishi miongoni mwa mataifa.” Wakazi wa Edomu, mwaweza kushangilia kwa sasa, mwaweza kwa sasa kufurahi enyi wakazi wa Uzi; lakini kikombe hiki cha adhabu kitawajia pia, nanyi pia mtakinywa na kulewa, hata mtayavua mavazi yenu! Adhabu ya uovu wako ewe Siyoni imekamilika; Mwenyezi-Mungu hatawaacha zaidi uhamishoni. Lakini nyinyi Waedomu atawaadhibu kwa uovu wenu, atazifichua dhambi zenu.