Mathayo 18:5-14
Mathayo 18:5-14 BHN
Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi. “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. “Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. Na jicho lako likikukosesha, lingoe na kulitupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili. “Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa. Nawaambieni, malaika wao huko mbinguni wako daima mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. [ Maana Mwana wa Mtu alikuja kuwaokoa wale waliopotea.] (Taz Luka 19:10). Mnaonaje? Mtu akiwa na kondoo 100, akimpoteza mmoja, hufanyaje? Huwaacha wale tisini na tisa mlimani, akaenda kumtafuta yule aliyepotea. Akimpata, nawaambieni kweli, humfurahia huyo kuliko awafurahiavyo wale tisini na tisa ambao hawakupotea. Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee.