Mathayo 28:8-15
Mathayo 28:8-15 BHN
Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake. Mara, Yesu akakutana nao, akasema: “Salamu.” Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake. Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona.” Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia. Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha wakisema, “Nyinyi mtasema hivi: ‘Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.’ Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa nyinyi hamtapata matatizo.” Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.