Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 11:1-11

Marko 11:1-11 BHN

Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwanapunda amefungwa, ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnafanya hivyo?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.’” Basi, wakaenda, wakamkuta mwanapunda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwanapunda?” Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. Wakampelekea Yesu huyo mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwanapunda na Yesu akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. Watu wote waliotangulia na wale waliofuata, wakapaza sauti zao wakisema, “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Ubarikiwe ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Sifa kwa Mungu juu mbinguni!” Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.