Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 17

17
1Afadhali mkate mkavu kwa amani,
kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi.
2Mtumwa mwenye busara atachukua nafasi ya mwana mpumbavu,
atapata sehemu ya urithi wa jamaa hiyo.
3Ubora wa dhahabu ama fedha hupimwa kwa moto,
lakini Mwenyezi-Mungu ndiye apimaye mioyo ya watu.
4Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya,
mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu.
5Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake;
anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa.
6Wazee huwaonea fahari wajukuu zao;
watoto huwaonea fahari wazazi wao.
7Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu,
sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi!
8Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi;
kila afanyacho hufanikiwa.
9Anayesamehe makosa hujenga urafiki,
lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki.
10Onyo kwa mwenye busara lina maana,
kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.
11Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu;
mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake.
12Afadhali kukutana na dubu jike aliyenyanganywa watoto wake,
kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake.
13Mwenye kulipiza mema kwa mabaya,
mabaya hayataondoka nyumbani mwake.
14Kuanzisha ugomvi ni kama kufanya ufa kwenye bwawa;
achana na ugomvi kabla haujafurika.
15Kumsamehe mwenye hatia na kumwadhibu asiye na hatia
yote mawili ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.
16Ya nini mpumbavu kuwa na fedha mkononi kununulia hekima,
wakati yeye mwenyewe hana akili?
17Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote,
ndugu huzaliwa asaidie wakati wa taabu.
18Si jambo la akili kuweka rehani,
na kuwa mdhamini wa mtu mwingine.
19Anayependa ugomvi anapenda dhambi;
anayejigamba#17:19 anayejigamba: Neno kwa neno; ainuaye sana mlango wake. anajitafutia maangamizi.
20Mwenye moyo mpotovu hafanikiwi,
na msema uongo hupatwa na maafa.
21Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake,
na baba wa mpumbavu hana furaha.
22Moyo mchangamfu ni dawa,
bali moyo wenye huzuni hudhoofisha mwili.
23Mtu mbaya hupokea hongo kwa siri
ili apate kupotosha haki.
24Mtu mwenye busara lengo lake ni hekima,
lakini mpumbavu hupania kila kitu duniani.
25Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake,
na uchungu kwa mama yake mzazi.
26Si vizuri kumtoza faini mtu asiye na hatia;
ni kosa kumchapa viboko muungwana.
27Asiyesema sana ana maarifa;
mtu mtulivu ni mwenye busara.
28Hata mpumbavu akinyamaza huonekana ana hekima;
akifunga mdomo wake huonekana kuwa mwenye akili.

Iliyochaguliwa sasa

Methali 17: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia