Methali 18
18
1Anayetafuta yake tu hujitenga na wenzake;
hukasirika akipewa shauri lolote jema.
2Mpumbavu hapendezwi na busara;
kwake cha maana ni maoni yake tu.
3Ajapo mwovu huja pia dharau;
pamoja na aibu huja fedheha.
4Maneno yaweza kuwa chemchemi ya hekima;
yenye kilindi kama bahari, kama kijito kinachobubujika.
5Si vizuri kumpendelea mtu mwovu,
na kumnyima haki mtu mwadilifu.
6Maneno ya mpumbavu huleta ugomvi;
kila anachosema husababisha adhabu.
7Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe;
mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe.
8Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu;
ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni.
9Mtu mvivu kazini mwake
ni ndugu yake mharibifu.
10Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara;
mwadilifu huukimbilia akawa salama.
11Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake;
anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda.
12Majivuno ya moyoni huleta maangamizi,
lakini unyenyekevu huleta heshima.
13Kujibu kabla ya kusikiliza
ni upumbavu na jambo la aibu.
14Roho ya mtu huweza kustahimili ugonjwa,
lakini ukiwa umevunjika moyo, utastahimilije?
15Mtu mwenye akili hujipatia maarifa,
sikio la mwenye busara hutafuta maarifa.
16Zawadi humfungulia mtu milango;
huweza kumfikisha mtu mbele ya mkuu.
17Ajiteteaye kwanza huonekana msema kweli,
mpaka hapo mpinzani wake atakapoanza kumhoji.
18Kura hukomesha ubishi;
huamua kati ya wakuu wanaopingana.
19Ndugu aliyeudhiwa ni mgumu kuliko mji wa ngome;#18:19 Ndugu … ngome: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
magomvi hubana kama makufuli ya ngome.
20Maneno ya mtu yaweza kumshibisha;
hutosheka kwa matokeo ya maneno yake.
21Ulimi una nguvu ya kufanya hai na kuua;
wanaopenda kuutumia watakula matunda yake.
22Anayempata mke amepata bahati njema;
hiyo ni fadhili kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
23Maskini huomba kwa unyenyekevu,
bali tajiri hujibu kwa ukali.
24Marafiki wengi waweza kumwangusha mtu,#18:24 Marafiki wengi … kumwangusha mtu: Maana yake katika makala ya Kiebrania si dhahiri.
lakini wapo marafiki waaminifu kuliko ndugu.
Iliyochaguliwa sasa
Methali 18: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.