Zaburi 135
135
Sifa kwa Mungu
1Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu,
msifuni enyi watumishi wake.
2Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake,
ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu!
3Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;
mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa.#135:3 maana inafaa: Au Maana ni mwema.
4Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake,
nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.
5Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu;
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.
6Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka,
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.
7Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia;
afanyaye gharika kuu kwa umeme,
na kuvumisha upepo kutoka ghala zake.
8Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri,
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.
9Ndiye aliyefanya ishara na maajabu kwako, ee Misri,
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.
10Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi,
akawaua wafalme wenye nguvu:
11Kina Sihoni mfalme wa Waamori,
Ogu mfalme wa Bashani,
na wafalme wote wa Kanaani.
12Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;
naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli.
13Jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele,
utakumbukwa kwa fahari nyakati zote.
14Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake;
na kuwaonea huruma watumishi wake.
15 # Taz Zab 115:4-8; Ufu 9:20 Miungu ya uongo ya mataifa ni fedha na dhahabu,
imetengenezwa kwa mikono ya binadamu.
16Ina vinywa, lakini haisemi;
ina macho, lakini haioni.
17Ina masikio, lakini haisikii;
wala haiwezi hata kuvuta pumzi.
18Wote walioifanya wafanane nayo,
naam, kila mmoja anayeitegemea!
19Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
Enyi makuhani, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
20Enyi Walawi, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
Enyi wachaji wa Mwenyezi-Mungu, mtukuzeni!
21Atukuzwe Mwenyezi-Mungu katika Siyoni,
atukuzwe katika makao yake Yerusalemu.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 135: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.