Zaburi 139:13-24
Zaburi 139:13-24 BHN
Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa. Umbo langu halikufichika kwako nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe. Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu! Laiti watu wauaji wangeondoka kwangu! Wanasema vibaya juu yako; wanasema maovu juu ya jina lako! Ee Mwenyezi-Mungu, nawachukia wanaokuchukia; nawadharau sana wale wanaokuasi! Maadui zako ni maadui zangu; ninawachukia kabisakabisa. Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele.