Zaburi 45:9-17
Zaburi 45:9-17 BHN
Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki, naye malkia amesimama kulia kwako, amevaa mapambo ya dhahabu safi ya Ofiri. Sikiliza binti, ufikirie! Tega sikio lako: Sahau sasa watu wako na jamaa zako. Uzuri wako wamvutia mfalme; yeye ni bwana wako, lazima umtii. Watu wa Tiro watakuletea zawadi; matajiri watataka upendeleo wako. Binti mfalme anaingia mzuri kabisa! Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu. Akiwa amevalia vazi la rangi nyingi, anaongozwa kwa mfalme, akisindikizwa na wasichana wenzake; nao pia wanapelekwa kwa mfalme. Kwa furaha na shangwe wanafika huko, na kuingia katika jumba la mfalme. Ee mfalme, utapata watoto wengi watakaotawala mahali pa wazee wako; utawafanya watawale duniani kote. Nitalifanya jina lako litukuzwe katika vizazi vyote, nayo mataifa yatakusifu daima na milele.