Zaburi 66
66
Wimbo wa shukrani
(Kwa Mwimbishaji. Wimbo. Zaburi)
1Enyi watu wote duniani mshangilieni Mungu!
2Imbeni juu ya utukufu wa jina lake,
mtoleeni sifa tukufu!
3Mwambieni Mungu: “Matendo yako ni ya ajabu mno!
Nguvu zako ni kubwa mno hata maadui zako wanajikunyata kwa hofu.
4Dunia yote inakuabudu;
watu wote wanakuimbia sifa!”
5Njoni mkaone mambo aliyotenda Mungu;
ametenda mambo ya kutisha kati ya watu:
6Aligeuza bahari kuwa nchi kavu,
watu wakapita humo kwa miguu;
hapo nasi tukashangilia kwa sababu yake.
7Anatawala milele kwa nguvu yake kuu;
macho yake huchungulia mataifa yote.
Mwasi yeyote asithubutu kumpinga.
8Msifuni Mungu wetu, enyi mataifa yote;
tangazeni sifa zake zipate kusikika.
9Yeye ametujalia maisha,
wala hakutuacha tuanguke.
10Umetupima, ee Mungu,
umetujaribu kama madini motoni.
11Umetuacha tunaswe wavuni;
umetubebesha taabu nzito.
12Umewaacha watu watukanyage;
tumepitia motoni na majini#66:12 Motoni na majini: Lugha ya picha inayoeleza magumu ya kupita kiasi, lakini yenye shabaha ya kutakasa..
Lakini sasa umetuleta kwenye usalama.
13Nitakuja nyumbani kwako na sadaka za kuteketezwa,
nitakutimizia nadhiri zangu,
14nilizotamka na kukuahidi mimi mwenyewe nilipokuwa taabuni.
15Nitakutolea sadaka za kuteketezwa nononono,
tambiko za kuteketezwa za kondoo madume;
nitatoa sadaka za ng'ombe na mbuzi.
16Enyi mnaomcha Mungu, njoni nyote mkasikilize,
nami nitawasimulieni aliyonitendea.
17Mimi nilimlilia msaada kwa sauti,
sifa zake nikazitamka.
18Kama ningalinuia maovu moyoni,
Mwenyezi-Mungu hangalinisikiliza.
19Lakini kweli Mungu amenisikiliza;
naam, amesikiliza maneno ya sala yangu.
20Asifiwe Mungu,
maana hakuikataa sala yangu,
wala kuondoa fadhili zake kwangu.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 66: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.