1 Wakorintho 10:14-22
1 Wakorintho 10:14-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu. Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo. Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo. Angalieni kwa mfano Wayahudi wenyewe: Wale wanaokula tambiko wanaungana na hiyo madhabahu. Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu? Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe nyinyi muwe na ushirika na pepo. Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika Karamu ya Bwana na katika meza ya pepo. Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye?
1 Wakorintho 10:14-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?
1 Wakorintho 10:14-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

1 Wakorintho 10:14-22 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa hiyo wapendwa wangu, zikimbieni ibada za sanamu. Nasema watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo. Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Al-Masihi? Mkate tunaoumega, si ushirika wa mwili wa Al-Masihi? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja. Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? Je, nina maana kwamba sadaka iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yoyote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yoyote? La hasha! Lakini sadaka za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana Isa na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika Chakula cha Bwana Isa na katika chakula cha mashetani pia. Je, tunataka kuamsha wivu wa Mwenyezi Mungu? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?