2 Samueli 16:1-14
2 Samueli 16:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Daudi alipokuwa amekipita kidogo kilele cha mlima, Siba mtumishi wa Mefiboshethi alimlaki Daudi akiwa na punda wawili ambao walikuwa wametandikwa huku wamebeba mikate200, vishada 100 vya zabibu kavu, matunda 100 ya kiangazi na kiriba cha divai. Mfalme akamwuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya kupanda jamaa yako, mikate na matunda ya kiangazi ni kwa ajili ya vijana wote, nayo divai ni kwa ajili ya watakaozimia jangwani.” Mfalme akamwuliza, “Mwana wa bwana wako yuko wapi?” Siba akamwambia mfalme, “Yeye amebaki mjini Yerusalemu kwa sababu anadhani kwamba watu wa Israeli watamrudishia ufalme wa Shauli babu yake.” Mfalme akamwambia Siba, “Basi, yale yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akamwambia, “Nashukuru, bwana wangu mfalme, nami naomba nipate fadhili mbele yako daima.” Wakati Daudi alipowasili kule Bahurimu, alitokea mtu mmoja wa ukoo wa Shauli, jina lake Shimei mwana wa Gera, akaanza kumlaani Daudi kwa mfululizo. Akawa anamtupia mfalme Daudi mawe pamoja na watumishi wake. Watu wengine wote na mashujaa wakawa wanamzunguka Daudi upande wa kulia na kushoto. Shimei alimlaani Daudi akisema, “Nenda zako; nenda zako, wewe mtu mwuaji, mtu asiye na faida! Mwenyezi-Mungu amekulipiza kisasi kutokana na kumwaga damu yote ya jamaa ya Shauli, ambaye sasa wewe umechukua ufalme mahali pake. Sasa, Mwenyezi-Mungu amempa ufalme Absalomu mwanao. Tazama, sasa maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mwuaji.” Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu akulaani wewe bwana wangu mfalme? Niruhusu nimwendee, nami nitakikata kichwa chake.” Lakini mfalme akamwambia, “Je, kuna nini kati yangu na nyinyi wana wa Seruya? Ikiwa Mwenyezi-Mungu amemwambia ‘Mlaani Daudi’, nani sasa anaweza kuuliza ‘Kwa nini umefanya hivyo?’” Tena mfalme Daudi akamwambia Abishai na hata watumishi wake wote, “Ikiwa mtoto wangu mwenyewe anayawinda maisha yangu, je si zaidi mtu wa kabila la Benyamini? Nyinyi mwacheni anilaani kwani Mwenyezi-Mungu amemwagiza anilaani. Huenda Mwenyezi-Mungu akaangalia uovu wangu, naye akanilipa wema kwa laana hii ninayopata leo.” Hivyo mfalme Daudi na watu wake wakaendelea na safari huku Shimei akiwa anamfuata akimtupia mawe na kurusha juu vumbi dhidi ya mfalme Daudi. Shimei alikuwa akitembea kileleni mwa mlima, mkabala na mfalme Daudi. Kisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakafika mtoni wakiwa wamechoka. Basi wakapumzika.
2 Samueli 16:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Daudi alipokipita punde hicho kilele cha mlima, tazama, Siba, mtumwa wa Mefiboshethi, akamkuta, na punda wawili waliotandikwa, na juu yao mikate mia mbili ya ngano, na vishada mia moja vya zabibu kavu, na matunda mia moja ya wakati wa joto, na kiriba cha divai. Mfalme akamwambia Siba, Ni za nini hizi? Siba akasema, Punda ni za jamaa ya mfalme wazipande; na mkate na matunda ni chakula cha hawa vijana; na divai ni kwamba wanywe hao wazimiao nyikani. Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa babu yangu. Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi ninasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme. Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kulia na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! BWANA amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye BWANA ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu BWANA amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya? Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; sembuse Mbenyamini huyu? Mwacheni alaani, kwa sababu BWANA ndiye aliyemwagiza. Labda BWANA atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye BWANA atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo. Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi. Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wakiwa wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.
2 Samueli 16:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Daudi alipokipita punde hicho kilele cha mlima, tazama, Siba, mtumwa wa Mefiboshethi, akamkuta, na punda wawili waliotandikwa, na juu yao mikate mia mbili ya ngano, na vishada mia vya zabibu kavu, na matunda mia ya wakati wa hari, na kiriba cha divai. Mfalme akamwambia Siba, Ni za nini hizi? Siba akasema, Punda ni za jamaa ya mfalme wazipande; na mkate na matunda ni chakula cha hawa vijana; na divai ni kwamba wanywe hao wazimiao nyikani. Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa baba yangu. Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi nasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme. Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! BWANA amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye BWANA ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu BWANA amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya? Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu BWANA ndiye aliyemwagiza. Labda BWANA atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye BWANA atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo. Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi. Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.
2 Samueli 16:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Daudi alipokuwa ameenda umbali mfupi kupita kilele cha mlima, akamkuta huko Siba, msimamizi wa shughuli za Mefiboshethi, akingojea kumlaki Daudi. Alikuwa na punda wawili wakiwa wametandikwa na kupakiwa mikate mia mbili, maandazi mia ya zabibu kavu, maandazi mia ya tini, na kiriba cha divai. Mfalme Daudi akamuuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya watu wa nyumba ya mfalme kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya watu kula, nayo divai ni kwa kuwaburudisha watakaochoka jangwani.” Kisha mfalme akauliza, “Yuko wapi mwana wa bwana wako?” Siba akamwambia, “Anakawia Yerusalemu, kwa sababu anafikiri, ‘Leo nyumba ya Israeli itanirudishia utawala wa baba yangu.’ ” Ndipo mfalme akamwambia Siba, “Yote yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akasema, “Nasujudu kwa unyenyekevu. Naomba nipate kibali mbele yako, bwana wangu mfalme.” Mfalme Daudi alipokuwa anakaribia Bahurimu, mtu mmoja wa ukoo wa jamaa ya Sauli, akatoka humo. Jina lake ni Shimei mwana wa Gera; akawa analaani alipokuwa akitoka. Akamtupia Daudi na maafisa wote wa mfalme mawe, ingawa vikosi vyote na walinzi maalum walikuwa kulia na kushoto mwa Daudi. Shimei alivyokuwa akilaani, akasema, “Toka hapa, toka hapa, wewe mtu wa damu, wewe mtu mbaya kabisa! Mwenyezi Mungu amekulipiza kwa ajili ya damu yote uliyomwaga ya watu wa nyumba ya Sauli, ambaye nafasi yake umeimiliki wewe. Mwenyezi Mungu amekabidhi ufalme mkononi mwa mwanao Absalomu. Maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mtu wa damu!” Ndipo Abishai mwana wa Seruya akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu amlaani bwana wangu mfalme? Niruhusu nivuke nikatilie mbali kichwa chake.” Lakini mfalme akamwambia, “Mna nini nami, enyi wana wa Seruya? Ikiwa analaani kwa sababu Mwenyezi Mungu amemwambia, ‘Mlaani Daudi,’ nani awezaye kuuliza, ‘Kwa nini unafanya hivi?’ ” Ndipo Daudi akamwambia Abishai na maafisa wake wote, “Mwanangu, ambaye ametoka viunoni mwangu mwenyewe, anajaribu kuniua. Je, si zaidi sana huyu Mbenyamini! Mwacheni; acha alaani, kwa maana Mwenyezi Mungu amemwambia afanye hivyo. Inawezekana kwamba Mwenyezi Mungu ataona dhiki yangu na kunilipa mema kwa ajili ya laana ninayopokea leo.” Kwa hiyo Daudi na watu wake wakaendelea na safari yao barabarani, huku Shimei akiwa anatembea pembezoni mwa kilima sambamba na Daudi, huku akimlaani na kumtupia Daudi mawe na kumrushia mavumbi. Mfalme na watu wote aliokuwa pamoja nao wakafika kwenye kituo chao wakiwa wamechoka. Mfalme akajiburudisha hapo.