Kutoka 21:1-11
Kutoka 21:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
“Haya ndiyo maagizo utakayowapa Waisraeli: Ukimnunua mtumwa Mwebrania, atakutumikia kwa miaka sita, lakini mwaka wa saba atakuwa huru na kuondoka, bila malipo. Kama alinunuliwa kabla hajaoa, ataondoka peke yake. Lakini kama alikuja na mkewe, basi, ataondoka na mkewe. Kama bwana wake alimwoza mke, akamzalia watoto wa kike au wa kiume, basi, huyo mwanamke na watoto wake watakuwa mali ya huyo bwana wake, na huyo mtumwa ataondoka peke yake. Lakini kama mtumwa huyo akisema kwamba anampenda bwana wake, mke wake na watoto wake na hataki kuondoka na kuwa huru, basi, bwana wake atamleta mbele ya Mungu. Kisha atampeleka kwenye mlango au kizingitini na kumtoboa sikio lake kwa shazia; naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote. “Mtu akimwuza binti yake kuwa mtumwa, huyo hatapata uhuru wake kama watumwa wa kiume. Ikiwa huyo bwana wake alimnunua awe mmoja wa wake zake, kisha asipendezwe naye, huyo bwana atamwacha baba yake huyo mtumwa amkomboe. Huyo bwana hana haki ya kumwuza kwa watu wa mataifa mengine, kwa kuwa atakuwa amekosa uaminifu. Kama ataamua kumwoza kwa mwanawe, atamtendea mtumwa huyo kama binti yake. Kama huyo bwana akioa mke mwingine, lazima aendelee kumtosheleza mkewe wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zake za ndoa. Iwapo huyo bwana hatamtimizia haki hizo tatu, basi, mke ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote.
Kutoka 21:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure. Ikiwa aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kama ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye. Ikiwa ni bwana wake aliyemwoza huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake. Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru; ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote. Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo. Ikiwa bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu. Akimposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake. Akijitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia. Ikiwa hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali.
Kutoka 21:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure. Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye. Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake. Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru; ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote. Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo. Kwamba bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu. Kwamba amposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake. Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia. Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali.
Kutoka 21:1-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Hizi ndizo sheria utakazoweka mbele ya Waisraeli. “Ukimnunua mtumwa Mwebrania, atakutumikia kwa miaka sita. Lakini katika mwaka wa saba, atakuwa huru naye ataenda zake pasipo kulipa chochote. Akija peke yake, ataenda huru peke yake, lakini akija na mke, ataondoka pamoja naye. Ikiwa bwana wake alimpatia mke naye akamzalia wana au binti, mwanamke pamoja na watoto wake watakuwa mali ya bwana wake, na huyo mwanaume ataondoka peke yake. “Lakini mtumishi akisema, ‘Ninampenda bwana wangu, mke wangu pamoja na watoto na sitaki kuwa huru,’ basi bwana wake atalazimika kumpeleka mbele ya waamuzi. Kisha atampeleka kwenye mlango, au kizingiti na kutoboa sikio lake kwa shazia. Naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote. “Mtu akimuuza binti yake kuwa mtumwa, hataachwa huru kama watumwa wa kiume wanavyoachiwa. Kama hakumpendeza bwana wake aliyemchagua, huyo bwana atamwacha akombolewe. Hatakuwa na haki ya kumuuza kwa wageni, kwa sababu huyo bwana atakuwa amekosa uaminifu. Akimchagua aolewe na mwanawe, ni lazima ampe haki za kuwa binti yake. Ikiwa huyo mwana aliyeozwa mtumwa mwanamke ataoa mwanamke mwingine, ni lazima aendelee kumtosheleza huyo mke wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zote za ndoa. Iwapo hatamtosheleza kwa mambo hayo matatu, huyo mke wa kwanza ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote ya fedha.