Kutoka 34:21-28
Kutoka 34:21-28 Biblia Habari Njema (BHN)
“Siku sita mtafanya kazi zenu, lakini siku ya saba mtapumzika, hata ikiwa ni wakati wa kulima au kuvuna. Mtaadhimisha sikukuu ya majuma mwanzoni mwa majira ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Nitayafukuza mataifa mengine mbele yenu na kuipanua mipaka yenu. Hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yenu wakati mnapokusanyika kuniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mara tatu kila mwaka. “Msinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na chachu; wala tambiko ya sikukuu ya Pasaka isibakizwe mpaka asubuhi. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Andika maneno haya, maana kulingana na maneno haya, ninafanya agano nawe na watu wa Israeli.” Mose alikaa huko mlimani pamoja na Mwenyezi-Mungu siku arubaini, mchana na usiku; hakula chakula wala kunywa maji. Aliandika maneno yote ya agano na zile amri kumi.
Kutoka 34:21-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika. Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka. Mara tatu kila mwaka wanaume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli. Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu yeyote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za BWANA Mungu wako mara tatu kila mwaka. Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya Pasaka haitasazwa hata asubuhi. Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya BWANA Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake. BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya. Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arubaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.
Kutoka 34:21-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika. Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka. Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli. Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za BWANA Mungu wako mara tatu kila mwaka. Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya pasaka haitasazwa hata asubuhi. Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya BWANA Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake. BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya. Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.
Kutoka 34:21-28 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike. “Utaadhimisha Sikukuu ya Majuma kwa malimbuko ya mavuno ya ngano, na Sikukuu ya Mavuno mwishoni mwa mwaka. Mara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele za Bwana Mungu Mwenyezi, Mungu wa Israeli. Nitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yako wakati unapoenda mara tatu kila mwaka kuonana na Mwenyezi Mungu, Mungu wako. “Usinitolee damu ya dhabihu pamoja na kitu chochote chenye chachu, wala usibakize dhabihu yoyote ya Sikukuu ya Pasaka hadi asubuhi. “Leta matunda ya kwanza yaliyo bora zaidi ya ardhi yako katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Andika maneno haya, kwa maana kulingana na maneno haya, nimefanya agano na wewe pamoja na Israeli.” Musa alikuwa huko pamoja na Mwenyezi Mungu kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya agano, yaani zile Amri Kumi.