Obadia 1:1-14
Obadia 1:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Maono ya Obadia. Mambo aliyosema Bwana Mwenyezi-Mungu kuhusu taifa la Edomu. Tumepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; mjumbe ametumwa kati ya mataifa: “Inukeni! Twende tukapigane na Edomu!” Mwenyezi-Mungu aliambia taifa la Edomu: “Nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, utadharauliwa kabisa na wote. Kiburi chako kimekudanganya: Kwa kuwa mji wako mkuu ni ngome ya miamba imara na makao yako yapo juu milimani, hivyo wajisemea, ‘Nani awezaye kunishusha chini?’ Hata ukiruka juu kama tai, ukafanya makao yako kati ya nyota, mimi nitakushusha chini tu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Kama wezi au wanyang'anyi wangekujia usiku, je, wasingechukua tu kiasi cha kuwatosha? Ikiwa wavunaji zabibu wangekujia, je, wasingekuachia kiasi kidogo tu? Lakini wewe, adui zako wamekuangamiza kabisa. Enyi wazawa wa Esau, mali zenu zimetekwa; hazina zenu zote zimeporwa! Washirika wenzenu wamewadanganya, wamewafukuza nchini mwenu. Mliopatana nao wamewashinda vitani, rafiki wa kutegemewa ndio waliokutegea mitego, nawe hukuelewa yaliyokuwa yanatendeka. Mimi Mwenyezi-Mungu nakuuliza hivi: Je, siku hiyo, sitawaangamiza wenye hekima kutoka Edomu na wenye maarifa kutoka mlima Esau? Ewe Temani, mashujaa wako watatishika na kila mtu atauawa mlimani Esau. “Kwa sababu ya matendo maovu mliyowatendea ndugu zenu wazawa wa Yakobo, mtaaibishwa na kuangamizwa milele. Siku ile mlisimama kando mkitazama tu, wakati wageni walipopora utajiri wao, naam, wageni walipoingia malango yao na kugawana utajiri wa Yerusalemu kwa kura. Kwa hiyo nanyi mlitenda kama wazawa wao. Msingalifurahia siku hiyo ndugu zenu walipokumbwa na mikasa; msingaliwacheka Wayuda na kuona fahari wakati walipoangamizwa; msingalijigamba wenzenu walipokuwa wanataabika. Msingeliingia katika mji wa watu wangu, siku walipokumbwa na maafa; msingelipora mali zao, siku hiyo ya maafa yao. Msingelisimama kwenye njia panda na kuwakamata wakimbizi wao; wala msingeliwakabidhi kwa adui zao wale waliobaki hai.
Obadia 1:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maono yake Obadia. Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu; Tumepata habari kwa BWANA, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Haya, inukeni ninyi; Na tuinuke tupigane naye. Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa; Umedharauliwa sana. Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kiota chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA. Kama wezi wangekujia, kama wanyang'anyi wangekujia usiku, (jinsi ulivyokatiliwa mbali!) Je! Wasingeiba kiasi cha kuwatosha? Kama wachumao zabibu wangekujia, je! Wasingeacha baadhi ya zabibu, ziokotwe? Jinsi watu wa Esau wanavyotafutwatafutwa! Jinsi hazina zake zilizofichwa zinavyoulizwaulizwa! Watu wote wa mapatano yako Wamekufukuza, hadi mipakani; Wale waliofanya amani nawe Wamekudanganya, na kukushinda; Walao mkate wako wameweka mtego chini yako; Wala hana ufahamu wa hayo ndani yake. Siku hiyo, je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu, na wenye ufahamu katika kilima cha Esau? Asema BWANA. Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau. Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele. Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpigia kura Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao. Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao. Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao. Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki.
Obadia 1:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maono yake Obadia. Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu; Tumepata habari kwa BWANA, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Haya, inukeni ninyi; Na tuinuke tupigane naye. Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa; Umedharauliwa sana. Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA. Kama wevi wangekujilia, kama wanyang’anyi wangekujilia usiku, (jinsi ulivyokatiliwa mbali!) Je! Wasingeiba kiasi cha kuwatosha? Kama wachumao zabibu wangekujilia, je! Wasingeacha baadhi ya zabibu, ziokotwe? Jinsi watu wa Esau wanavyotafutwa-tafutwa! Jinsi hazina zake zilizofichwa zinavyoulizwa-ulizwa! Watu wote wa mapatano yako Wamekufukuza, hata mipakani; Wale waliofanya amani nawe Wamekudanganya, na kukushinda; Walao mkate wako wameweka mtego chini yako; Wala hana ufahamu wa hayo ndani yake. Siku hiyo, je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu, na wenye ufahamu katika kilima cha Esau? Asema BWANA. Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau. Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele. Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao. Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao. Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao. Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki.
Obadia 1:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Maono ya Obadia. Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu Edomu: Tumesikia ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Inukeni, twendeni tukapigane vita dhidi yake.” “Tazama, nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, utadharauliwa kabisa. Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, wewe unayeishi katika mapango ya miamba na kufanya makao yako juu, wewe unayejiambia mwenyewe, ‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’ Ingawa unapaa juu kama tai na kufanya kiota chako kati ya nyota, nitakushusha chini kutoka huko,” asema Mwenyezi Mungu. “Ikiwa wezi wangekuja kwako, ikiwa wanyang’anyi wangekujia usiku: Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yanakungojea: je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji? Kama wachuma zabibu wangekuja kwako, je, wasingebakiza zabibu chache? Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa, jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara! Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani, rafiki zako watakudanganya na kukushinda, wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego, lakini hutaweza kuugundua. “Katika siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu, “je, sitaangamiza wenye hekima wa Edomu, hao wenye ufahamu katika milima ya Esau? Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu, kila mmoja katika milima ya Esau ataangushwa chini kwa kuchinjwa. Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika; utaangamizwa milele. Siku ile ulisimama mbali ukiangalia wakati wageni walipojichukulia utajiri wake, na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu, ulikuwa kama mmoja wao. Usingemdharau ndugu yako katika siku ya msiba wake, wala kufurahia juu ya watu wa Yuda katika siku ya maangamizi yao, wala kujigamba sana katika siku ya taabu yao. Usingeingia katika malango ya watu wangu katika siku ya maafa yao, wala kuwadharau katika janga lao katika siku ya maafa yao, wala kunyang’anya mali yao katika siku ya maafa yao. Usingengoja kwenye njia panda na kuwaua wakimbizi wao, wala kuwatoa watu wake waliosalia katika siku ya shida yao.