Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Obadia 1:1-14

Obadia 1:1-14 BHN

Maono ya Obadia. Mambo aliyosema Bwana Mwenyezi-Mungu kuhusu taifa la Edomu. Tumepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; mjumbe ametumwa kati ya mataifa: “Inukeni! Twende tukapigane na Edomu!” Mwenyezi-Mungu aliambia taifa la Edomu: “Nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, utadharauliwa kabisa na wote. Kiburi chako kimekudanganya: Kwa kuwa mji wako mkuu ni ngome ya miamba imara na makao yako yapo juu milimani, hivyo wajisemea, ‘Nani awezaye kunishusha chini?’ Hata ukiruka juu kama tai, ukafanya makao yako kati ya nyota, mimi nitakushusha chini tu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Kama wezi au wanyang'anyi wangekujia usiku, je, wasingechukua tu kiasi cha kuwatosha? Ikiwa wavunaji zabibu wangekujia, je, wasingekuachia kiasi kidogo tu? Lakini wewe, adui zako wamekuangamiza kabisa. Enyi wazawa wa Esau, mali zenu zimetekwa; hazina zenu zote zimeporwa! Washirika wenzenu wamewadanganya, wamewafukuza nchini mwenu. Mliopatana nao wamewashinda vitani, rafiki wa kutegemewa ndio waliokutegea mitego, nawe hukuelewa yaliyokuwa yanatendeka. Mimi Mwenyezi-Mungu nakuuliza hivi: Je, siku hiyo, sitawaangamiza wenye hekima kutoka Edomu na wenye maarifa kutoka mlima Esau? Ewe Temani, mashujaa wako watatishika na kila mtu atauawa mlimani Esau. “Kwa sababu ya matendo maovu mliyowatendea ndugu zenu wazawa wa Yakobo, mtaaibishwa na kuangamizwa milele. Siku ile mlisimama kando mkitazama tu, wakati wageni walipopora utajiri wao, naam, wageni walipoingia malango yao na kugawana utajiri wa Yerusalemu kwa kura. Kwa hiyo nanyi mlitenda kama wazawa wao. Msingalifurahia siku hiyo ndugu zenu walipokumbwa na mikasa; msingaliwacheka Wayuda na kuona fahari wakati walipoangamizwa; msingalijigamba wenzenu walipokuwa wanataabika. Msingeliingia katika mji wa watu wangu, siku walipokumbwa na maafa; msingelipora mali zao, siku hiyo ya maafa yao. Msingelisimama kwenye njia panda na kuwakamata wakimbizi wao; wala msingeliwakabidhi kwa adui zao wale waliobaki hai.

Soma Obadia 1