Oba 1:1-14
Oba 1:1-14 SUV
Maono yake Obadia. Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu; Tumepata habari kwa BWANA, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Haya, inukeni ninyi; Na tuinuke tupigane naye. Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa; Umedharauliwa sana. Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA. Kama wevi wangekujilia, kama wanyang’anyi wangekujilia usiku, (jinsi ulivyokatiliwa mbali!) Je! Wasingeiba kiasi cha kuwatosha? Kama wachumao zabibu wangekujilia, je! Wasingeacha baadhi ya zabibu, ziokotwe? Jinsi watu wa Esau wanavyotafutwa-tafutwa! Jinsi hazina zake zilizofichwa zinavyoulizwa-ulizwa! Watu wote wa mapatano yako Wamekufukuza, hata mipakani; Wale waliofanya amani nawe Wamekudanganya, na kukushinda; Walao mkate wako wameweka mtego chini yako; Wala hana ufahamu wa hayo ndani yake. Siku hiyo, je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu, na wenye ufahamu katika kilima cha Esau? Asema BWANA. Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau. Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele. Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao. Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao. Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao. Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki.