Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Obadia 1

1
1Maono ya Obadia.
Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu Edomu:
Tumesikia ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema,
“Inukeni, twendeni tukapigane vita dhidi yake.”
2“Tazama, nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa,
utadharauliwa kabisa.
3Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,
wewe unayeishi katika mapango ya miamba
na kufanya makao yako juu,
wewe unayejiambia mwenyewe,
‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’
4Ingawa unapaa juu kama tai
na kufanya kiota chako kati ya nyota,
nitakushusha chini kutoka huko,”
asema Mwenyezi Mungu.
5“Ikiwa wezi wangekuja kwako,
ikiwa wanyang’anyi wangekujia usiku:
Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yanakungojea:
je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji?
Kama wachuma zabibu wangekuja kwako,
je, wasingebakiza zabibu chache?
6Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa,
jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara!
7Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani,
rafiki zako watakudanganya na kukushinda,
wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego,
lakini hutaweza kuugundua.
8“Katika siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu,
“je, sitaangamiza wenye hekima wa Edomu,
hao wenye ufahamu katika milima ya Esau?
9Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu,
kila mmoja katika milima ya Esau
ataangushwa chini kwa kuchinjwa.
10Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo,
aibu itakufunika;
utaangamizwa milele.
11Siku ile ulisimama mbali ukiangalia
wakati wageni walipojichukulia utajiri wake,
na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake
wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu,
ulikuwa kama mmoja wao.
12Usingemdharau ndugu yako
katika siku ya msiba wake,
wala kufurahia juu ya watu wa Yuda
katika siku ya maangamizi yao,
wala kujigamba sana
katika siku ya taabu yao.
13Usingeingia katika malango ya watu wangu
katika siku ya maafa yao,
wala kuwadharau katika janga lao
katika siku ya maafa yao,
wala kunyang’anya mali yao
katika siku ya maafa yao.
14Usingengoja kwenye njia panda
na kuwaua wakimbizi wao,
wala kuwatoa watu wake waliosalia
katika siku ya shida yao.
15“Siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu
kwa mataifa yote.
Kama ulivyotenda, nawe utatendewa vivyo hivyo,
matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako.
16Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu,
vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo;
watakunywa na kunywa,
nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo.
17Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwa na wale watakaookoka;
nao utakuwa mtakatifu,
nayo nyumba ya Yakobo
itamiliki urithi wake.
18Nyumba ya Yakobo itakuwa moto,
na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto;
nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu,
nao wataiwasha moto na kuiteketeza.
Hakutakuwa na watakaosalimika
kutoka nyumba ya Esau.”
Mwenyezi Mungu amesema.
19Watu kutoka nchi ya Negebu
wataimiliki milima ya Esau,
na watu kutoka Shefela#1:19 au upande wa magharibi chini ya vilima
wataimiliki nchi ya Wafilisti.
Watayamiliki mashamba ya Efraimu na Samaria,
naye Benyamini atamiliki Gileadi.
20Kundi la Waisraeli walio uhamishoni Kanaani
watarudi na kuimiliki nchi hadi Sarepta.
Walio uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu
wataimiliki miji ya Negebu.
21Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni
kutawala milima ya Esau.
Nao ufalme utakuwa wa Mwenyezi Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Obadia 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia