Zaburi 31:1-8
Zaburi 31:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwako, ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama, usiniache niaibike kamwe; kwa uadilifu wako uniokoe. Unitegee sikio, uniokoe haraka! Uwe kwangu mwamba wa usalama, ngome imara ya kuniokoa. Naam, wewe ni mwamba wangu na ngome yangu; kwa hisani yako uniongoze na kunielekeza. Unitoe katika mtego walionitegea mafichoni; maana wewe ni kimbilio la usalama wangu. Mikononi mwako naiweka roho yangu; umenikomboa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwaminifu. Wawachukia wanaoabudu sanamu batili; lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu. Nitashangilia na kufurahia fadhili zako, maana wewe waiona dhiki yangu, wajua na taabu ya nafsi yangu. Wewe hukuniacha nitiwe mikononi mwa maadui zangu; umenisimamisha mahali pa usalama.
Zaburi 31:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Ngome thabiti ya kuniokoa. Ndiwe mwamba wangu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze na unichunge. Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu. Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli. Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumainia BWANA. Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni, Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha mahali penye usalama.
Zaburi 31:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Nyumba yenye maboma ya kuniokoa. Ndiwe genge langu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu. Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli. Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumaini BWANA. Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni, Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.
Zaburi 31:1-8 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe, kwa haki yako uniokoe. Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka; uwe kwangu mwamba wa kimbilio, ngome imara ya kuniokoa. Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu, uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako. Uniepushe na mtego niliotegewa, maana wewe ndiwe kimbilio langu. Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako, unikomboe Ee Mwenyezi Mungu, uliye Mungu wa kweli. Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili; bali mimi ninamtumaini Mwenyezi Mungu. Nitafurahia na kushangilia upendo wako, kwa kuwa uliona mateso yangu na ulijua maumivu ya nafsi yangu. Hukunikabidhi kwa adui yangu bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.