UTANGULIZI
Injili ilivyoandikwa na Yohane inatuhabarisha kwamba Yesu ni Neno la Mungu ambaye, alikuja duniani, akawa mwanadamu, akakaa kwetu (1:14). Kama kitabu chenyewe kinavyotuambia, Injili hii iliandikwa ili wasomaji wake wapate kuamini kwamba Yesu ndiye Mwokozi, Mwana wa Mungu, na kwamba kwa kumtegemea yeye, yaani kumwamini, watu watapata uhai (20:31).
Kwanza tunapewa utangulizi ambao unaonesha dhahiri kwamba Yesu ndiye Neno la Mungu, kisha tunahabarishwa juu ya miujiza kadhaa ambayo shabaha yake ni kuonesha kwamba Yesu ndiye Mwokozi ambaye Mungu aliahidi kumtuma duniani; yeye ndiye Mwana wa Mungu. Tunaambiwa jinsi watu kadhaa walivyomwamini Yesu, wakawa wafuasi wake, hali wengine walimpinga, wakakataa kumwamini.
Sura 13–17 zinaonesha kinaganaga uhusiano wa pekee kati ya Yesu na wafuasi wake; na kutupatia maneno yake ya kuwafariji na kuwapa moyo kabla ya kusulubiwa kwake. Sura zinazofuata zinaeleza juu ya kukamatwa kwa Yesu, kuhukumiwa, kusulubiwa, kufufuka na kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka.
Sura 7:53–8:11 imetiwa katika mabano ya mraba kwa kuwa makala nyingi muhimu za kale na tafsiri nyingine za awali hazina sehemu hiyo, hali nyingine zina sehemu hiyo mahali pengine.
Injili ya Yohane inatilia mkazo jambo la uhai wa milele ambao wapatikana kwa njia ya Yesu Kristo. Uhai huo wa milele ni zawadi kwa wale wanaomkubali Kristo Yesu, aliye njia, ukweli na uhai wetu.
Kwa namna ya pekee Yohane anatuelezea mambo muhimu katika maisha ya Yesu kwa kutumia vielelezo kutokana na maisha ya kawaida kuelezea maisha ya kiroho: Maji, chakula, mwanga, mchungaji, mkulima, n.k.
Injili kama ilivyoandikwa na Yohane inatofautiana sana na Injili zile nyingine tatu. Sura 18–19 ambazo zinazungumzia mateso ya Yesu ndizo zinazolingana na habari tunayopewa katika Injili zile nyingine. Injili hii ndiyo peke yake inayotupa habari kadhaa kama vile harusi mjini Kana (2:1-12), mazungumzo ya Yesu na Nikodemo (3:1-21), mazungumzo na mama Msamaria (4:1-42), kisa cha kilema wa Bethzatha (5:1-18), mtu aliyezaliwa kipofu (9:1-41). Visa hivyo vinafuatiwa na maelezo maalumu au mafundisho anayotoa Yesu. Yohane hutofautiana na waandishi wa Injili nyingine tatu zilizotangulia kwa namna namna:
1. Katika Sunoptiki Wanafunzi wanachukua muda mrefu kumtambua na kumwamini Yesu kama Masiha, Mwana wa Mungu (Marko 5:27 na sehemu sambamba). Katika Yohane hayo yanafanyika mara wanapokutana naye kwa mara ya kwanza (1:29-36,41,45,49; 4:29; 4:42) wote wahusika wanamtambua Yesu na kukiri (kuungama) kuwa Mwanakondoo wa Mungu, Masiha, Mwokozi aliyebashiriwa katika Maandiko Matakatifu, Mwokozi wa Ulimwengu.
2. Katika Sunoptiki, Yesu anafundisha kwa jumla kwa kutumia mfano. Yohane anatupa picha ya Yesu anafundisha kwa maelezo yake mwenyewe na mahojiano na watu ambavyo vyote vyazingatia uhusiano wake na Mungu Baba.
3. Nadharia kuu katika Sunoptiki ni ufalme wa Mungu; katika Yohane ni uhai wa milele (3:15,16,36; 4:14,36; 5:24,39; 6:27,40,47,54,68; 10:28; 12:25,50; 17:2,3).
4. Nafasi ya Roho Mtakatifu katika Injili hii ni karibu kama katika Sunoptiki. Lakini katika Yohane zaidi ya Sunoptiki Roho Mtakatifu ni Msaidizi ambaye Mungu atamtuma kuchukua nafasi ya Yesu (14:15-17; 14:25-26; 15:26; 16:7-11; 16:12-15). Jukumu kuu la Msaidizi ni kuwaongoza wanafunzi kwenye ukweli (16:13) na mwishoni Yesu anawapulizia (20:22,23; Taz 7:39).
5. Tofauti na Sunoptiki Injili hii ina tamko muhimu “Mimi ndimi” ambalo linatokea mara nyingi hasa katika sehemu ambazo Yesu anatenda “ishara”. Yesu ni mkate wa uhai (6:35), mwanga wa ulimwengu (18:18), mlango wa kondoo (11:25) njia, ukweli na uhai (14:6).