Yohana 7

7
Kutokuamini Kwa Ndugu Zake Yesu
1 Baada ya mambo haya, Yesu alikwenda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Uyahudi kwa sababu Wayahudi huko walitaka kumuua. 2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. 3 Hivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Uyahudi ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya. 4Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jionyeshe kwa ulimwengu.” 5 Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.
6 Yesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote. 7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu. 8 Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.” 9Akiisha kusema hayo, akabaki Galilaya.
Yesu Kwenye Sikukuu Ya Vibanda
10Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri. 11 Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”
12 Kulikuwa na minongʼono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”
Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.” 13 Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kumhusu kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.
Yesu Afundisha Kwenye Sikukuu
14 Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. 15 Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”
16 Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. 17 Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. 19 Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
20 Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”
21 Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. 22 Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. 23 Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? 24 Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”
Je, Yesu Ndiye Kristo?
25 Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua? 26 Mbona yuko hapa anazungumza hadharani na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo?#7:26 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. 27 Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”
28 Ndipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui. 29 Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”
30 Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia. 31 Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu zaidi kuliko aliyoifanya mtu huyu?”
Walinzi Wanatumwa Kumkamata Yesu
32Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.
33 Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. 34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”
35 Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani? 36 Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”
Mito Ya Maji Ya Uzima
37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.” 39 Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.
Mgawanyiko Miongoni Mwa Watu
40 Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”
41 Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!”
Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya? 42 Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?” 43 Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu. 44 Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.
Kutokuamini Kwa Viongozi Wa Wayahudi
45 Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”
46 Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”
47 Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika? 48 Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini? 49Lakini huu umati wa watu wasiojua Sheria ya Mose, wamelaaniwa.”
50 Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Yesu siku moja usiku, ambaye alikuwa mmoja wao akauliza, 51 “Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”
52 Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!” [ 53Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani kwake.

Currently Selected:

Yohana 7: NEN

Qaqambisa

Share

Copy

None

Ufuna ukuba iimbalasane zakho zigcinwe kuzo zonke izixhobo zakho? Bhalisela okanye ngena