YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 139

139
Zaburi 139
Mwenyezi Mungu asiyeweza kukwepwa
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1Ee Mwenyezi Mungu, umenichunguza
na kunijua.
2Unajua ninapoketi na ninapoinuka;
unatambua mawazo yangu tokea mbali.
3Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;
unaelewa njia zangu zote.
4Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,
wewe walijua kikamilifu, Ee Mwenyezi Mungu.
5Umenizingira nyuma na mbele;
umeweka mkono wako juu yangu.
6Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,
ni ya juu sana kwangu kuyafikia.
7Niende wapi nijiepushe na Roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
8Nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;
nikifanya vilindi#139:8 Vilindi ina maana ya Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol. kuwa kitanda changu,
wewe uko huko.
9Nikipanda juu kwa mabawa ya mapambazuko,
nikikaa pande za mbali za bahari,
10hata huko mkono wako utaniongoza,
mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.
11Nikisema, “Hakika giza litanificha
na nuru inayonizunguka iwe usiku,”
12hata giza halitakuwa giza kwako,
usiku utang’aa kama mchana,
kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
13Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;
uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
14Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa
kwa namna ya ajabu na ya kutisha;
kazi zako ni za ajabu,
ninajua hayo kikamilifu.
15Umbile langu halikufichika kwako,
nilipoumbwa mahali pa siri.
Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
16macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.
Siku zangu zote ulizonipangia
ziliandikwa katika kitabu chako
kabla haijakuwa hata moja.
17Tazama jinsi yalivyo ya thamani
mawazo yako kwangu, Ee Mungu!
Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!
18Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi
kuliko mchanga:
niamkapo, bado niko pamoja nawe.
19Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu!
Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!
20Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya,
adui zako wanatumia vibaya jina lako.
21Ee Mwenyezi Mungu, je, nisiwachukie wanaokuchukia?
Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?
22Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao,
ninawahesabu ni adui zangu.
23Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,
nijaribu na ujue mawazo yangu.
24Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,
uniongoze katika njia ya milele.

Currently Selected:

Zaburi 139: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in