Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 11:26-43

1 Wafalme 11:26-43 NEN

Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Solomoni, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua. Haya ndiyo maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Solomoni alikuwa amejenga Milo naye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake. Basi Yeroboamu alikuwa mtu shujaa na hodari, naye Solomoni alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yosefu. Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani, naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili. Kisha akamwambia Yeroboamu, “Chukua vipande kumi kwa ajili yako, kwa kuwa hivi ndivyo BWANA, Mungu wa Israeli asemavyo: ‘Tazama, ninakwenda kuuchana ufalme kutoka mikononi mwa Solomoni na kukupa wewe makabila kumi. Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja. Nitafanya hivi kwa sababu wameniacha mimi na kuabudu Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakwenda katika njia zangu ili kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Solomoni, alivyofanya. “ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote kutoka mikononi mwa Solomoni, nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu. Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi. Nitampa mwanawe kabila moja ili kwamba Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu. Hata hivyo, kukuhusu wewe Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala juu ya yote yale moyo wako unayotamani, utakuwa mfalme juu ya Israeli. Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kuzishika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ufalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli. Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya hili, lakini siyo milele.’ ” Solomoni akajaribu kumuua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki. Kwa habari za matukio mengine ya utawala wa Solomoni, yote aliyoyafanya na hekima aliyoionyesha, je hayakuandikwa yote katika kitabu cha matendo cha Solomoni? Solomoni alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu. Kisha Solomoni akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 11:26-43