Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 11:26-43

1 Wafalme 11:26-43 SRUV

Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akamwasi mfalme. Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwasi mfalme. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi. Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu. Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe makabila kumi, (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya makabila ya Israeli); kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake. Lakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; bali nitamfanya awe mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu, ila nitauondoa ufalme katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe makabila kumi. Nami nitampa mwana wake kabila moja, ili Daudi, mtumishi wangu, apate kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu, mji ule niliouchagua niweke jina langu huko. Nami nitakutwaa wewe, nawe utatawala kama roho yako inavyotamani, nawe utakuwa mfalme juu ya Israeli. Tena itakuwa, ukiyasikia yote nitakayokuamuru, na kuenda katika njia zangu, na kutenda yaliyo mema machoni pangu, ili kuzishika amri zangu na hukumu zangu kama Daudi mtumishi wangu alivyotenda, basi, nitakuwa pamoja nawe, nitakujengea nyumba iliyo imara, kama nilivyomjengea Daudi, nami nitakupa wewe Israeli. Tena nitawatesa wazao wa Daudi kwa sababu hii, lakini si daima. Basi Sulemani akataka kumwua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akaondoka, akakimbilia Misri, kwa Shishaki, mfalme wa Misri, akakaa katika Misri hata wakati wa kufa kwake Sulemani. Nayo yaliyosalia ya Sulemani, mambo yake na yote aliyoyafanya, na hekima yake, je! Hayo siyo yaliyoandikwa kitabuni mwa mambo yake Sulemani? Na siku alizotawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote zilikuwa miaka arubaini. Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi baba yake; na Rehoboamu mwanawe akatawala mahali pake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 11:26-43