1 Wafalme 14:1-11
1 Wafalme 14:1-11 NENO
Wakati ule, Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua, naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme wa watu hawa, yuko huko. Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.” Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama mumewe alivyosema, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo. Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake. Lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.” Hivyo, Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa si wewe? Nimetumwa kwako kukupa habari mbaya. Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli. Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu. Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunigeuka. “ ‘Kwa sababu hii, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu hadi iteketee yote kama mtu anavyochoma kinyesi. Mbwa watawala walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani. Mwenyezi Mungu amenena!’