Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 14:1-11

1 Fal 14:1-11 SUV

Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu. Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje. Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake. BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine. Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito. Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli, nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu; lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako; tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia. Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo.