1 Timotheo 3
3
Sifa za waangalizi
1Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kuwa mwangalizi wa kundi la waumini, atamani kazi nzuri. 2Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5(Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kundi la waumini la Mungu?) 6Asiwe mtu aliyeongoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi. 7Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.
Sifa za mashemasi
8Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. 9Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. 10Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.
11Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.
12Shemasi awe mume wa mke mmoja, na aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. 13Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Al-Masihi Isa.
14Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili, 15nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo jumuiya ya waumini ya Mungu aliye hai, iliyo nguzo na msingi wa kweli. 16Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa:
Alidhihirishwa katika mwili,
akathibitishwa kuwa na haki katika Roho wa Mungu,
akaonekana na malaika,
akahubiriwa miongoni mwa mataifa,
akaaminiwa ulimwenguni,
akachukuliwa juu katika utukufu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Timotheo 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.