2 Samweli 8:1-18
2 Samweli 8:1-18 NENO
Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akatwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti. Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili, hilo kundi waliuawa, na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea ushuru. Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipoenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati. Daudi akateka magari yake ya vita elfu moja, waendesha hayo magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu ishirini. Daudi akawakata mishipa farasi wa magari ya vita, akabakiza farasi mia moja. Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua watu elfu ishirini na mbili miongoni mwao. Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kote alipoenda. Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. Kutoka miji ya Tibathi na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana. Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba. Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda: yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi. Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Mwenyezi Mungu alimpatia Daudi ushindi kila alipoenda. Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu; Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.