2 Samueli 8:1-18
2 Samueli 8:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo, Daudi aliwapiga, akawashinda Wafilisti. Akauteka mji wa Metheg-ama kutoka utawala wa Wafilisti. Kisha aliwashinda Wamoabu. Aliwapanga katika mistari mateka hao, na kuwalaza chini. Aliamuru wale waliokuwa katika mistari miwili wauawe na wale wa mstari wa tatu waachwe hai. Hivyo, Wamoabu wakawa watumishi wake Daudi na wakawa wanamlipa kodi. Daudi pia alimshinda Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Daudi alipata ushindi huu wakati Hadadezeri alipokuwa njiani kwenda kulirudisha eneo la mto Eufrate kuwa chini ya utawala wake. Daudi aliteka wapandafarasi 1,700, na askari wa miguu 20,000. Kisha Daudi alikata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wa magari, ila alibakiza farasi wa kutosheleza magari 100. Nao Waaramu wa Damasko walipokwenda kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi aliwashambulia na kuwaua watu 22,000. Halafu Daudi aliweka kambi za kijeshi katika mji wa Waaramu wa Damasko. Basi, Waaramu wakawa watumishi wake na wakawa wanamlipa kodi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri na kuzipeleka Yerusalemu. Pia alichukua shaba nyingi sana kutoka miji ya Beta na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri. Wakati Toi, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, alimtuma mwanawe Yoramu kwa mfalme Daudi kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Toi mara nyingi. Yoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba. Zawadi hizo, pamoja na fedha na dhahabu alizokuwa ameziteka kwa mataifa yote aliyoyashinda, aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, yaani kutoka Edomu, Moabu, Amoni, Filistia, Amaleki, pamoja na nyara alizoteka kwa mfalme Hadadezeri, mwana wa Rehobu mfalme wa Soba. Daudi alijiongezea umaarufu wake. Alipokuwa anarudi baada ya kumshinda Hadadezeri, aliwaua Waedomu 18,000, katika Bonde la Chumvi. Akaweka kambi za kijeshi katika Edomu yote. Nao Waedomu wote wa huko wakawa watumishi wake. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Hivyo, Daudi akatawala juu ya Israeli yote, akahakikisha watu wake wote wanatendewa haki ipasavyo. Yoabu mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa majeshi. Yehoshafati mwana wa Ahiludi, alikuwa mweka kumbukumbu. Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani. Seraya alikuwa katibu. Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa kiongozi wa Wakerethi na Wapelethi, nao wana wa Daudi wakawa makuhani.
2 Samueli 8:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda; Daudi akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa hao Wafilisti. Akapiga Moabu, akawapima kwa kamba wakiwa wamelazwa chini; akapima kamba mbili za kuuawa, na kamba moja nzima ya kuhifadhi hai. Wamoabi wakawa watumishi wa Daudi, wakaleta zawadi. Tena Daudi akampiga Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kujipatia tena mamlaka yake huko Mtoni. Daudi akampokonya wapanda farasi elfu moja na mia saba na askari waliokwenda kwa miguu elfu ishirini; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila farasi wa magari mia moja akawabakiza. Na Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akawapiga watu elfu ishirini na mbili wa Washami. Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumishi wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu. Tena toka Tebhathi na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno. Na Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia ya kwamba Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, Tou akamtuma Yoramu mwanawe kwa mfalme Daudi ili kumsalimia, na kumpongeza, na kumbariki, kwa sababu amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou. Na mkononi mwake Yorabu akaleta vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na vyombo vya shaba; hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha, na dhahabu alizofanya wakfu za mataifa yote aliowashinda; za Edomu, na za Moabu, na za wana wa Amoni, na za Wafilisti, na za Amaleki, na za nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Basi Daudi akajipatia jina, alipokuwa akirudi, aliwaua Waedomi elfu kumi na nne katika bonde la chumvi. Akaweka askari wenye kulinda ngome katika Edomu; katikati ya Edomu yote akaweka ngome, na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi ushindi kila kokote alikokwenda. Daudi akatawala juu ya Israeli wote; naye Daudi akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. Huyo Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa majeshi; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, mwekaji kumbukumbu; na Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi wakawa makuhani.
2 Samueli 8:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda; Daudi akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa hao Wafilisti. Akapiga Moabu, akawapima kwa kamba hali wamelazwa chini; akapima kamba mbili za kuuawa, na kamba moja nzima ya kuhifadhi hai. Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Tena Daudi akampiga Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kujipatia tena mamlaka yake huko Mtoni. Daudi akampokonya wapanda farasi elfu na mia saba na askari waliokwenda kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila farasi wa magari mia akawasaza. Na Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akawapiga wa Washami watu ishirini na mbili elfu. Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumwa wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu. Tena toka Tebhathi na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno. Na Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia ya kwamba Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, Tou akamtuma kwa Daudi Hadoramu mwanawe kusalimia, na kumbarikia, kwa sababu amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou. Na mkononi mwake akaleta vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na vyombo vya shaba; hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha, na dhahabu alizofanya wakfu za mataifa yote aliowashinda; za Edomu, na za Moabu, na za wana wa Amoni, na za Wafilisti, na za Amaleki, na za nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Basi Daudi akajipatia jina, aliporudi kutoka kuwapiga Waedomi katika Bonde la Chumvi, watu kumi na nane elfu. Akaweka askari wenye kulinda ngome katika Edomu; katikati ya Edomu yote akaweka ngome, na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Daudi akatawala juu ya Israeli wote; naye Daudi akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. Huyo Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa juu ya jeshi; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, mwenye kuandika tarehe; na Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi wakawa makuhani.
2 Samueli 8:1-18 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akatwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti. Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili, hilo kundi waliuawa, na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea ushuru. Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipoenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati. Daudi akateka magari yake ya vita elfu moja, waendesha hayo magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu ishirini. Daudi akawakata mishipa farasi wa magari ya vita, akabakiza farasi mia moja. Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua watu elfu ishirini na mbili miongoni mwao. Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kote alipoenda. Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. Kutoka miji ya Tibathi na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana. Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba. Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda: yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi. Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Mwenyezi Mungu alimpatia Daudi ushindi kila alipoenda. Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu; Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.