2 Samweli 8:1-18
2 Samweli 8:1-18 SRUV
Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda; Daudi akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa hao Wafilisti. Akapiga Moabu, akawapima kwa kamba wakiwa wamelazwa chini; akapima kamba mbili za kuuawa, na kamba moja nzima ya kuhifadhi hai. Wamoabi wakawa watumishi wa Daudi, wakaleta zawadi. Tena Daudi akampiga Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kujipatia tena mamlaka yake huko Mtoni. Daudi akampokonya wapanda farasi elfu moja na mia saba na askari waliokwenda kwa miguu elfu ishirini; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila farasi wa magari mia moja akawabakiza. Na Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akawapiga watu elfu ishirini na mbili wa Washami. Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumishi wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu. Tena toka Tebhathi na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno. Na Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia ya kwamba Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, Tou akamtuma Yoramu mwanawe kwa mfalme Daudi ili kumsalimia, na kumpongeza, na kumbariki, kwa sababu amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou. Na mkononi mwake Yorabu akaleta vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na vyombo vya shaba; hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha, na dhahabu alizofanya wakfu za mataifa yote aliowashinda; za Edomu, na za Moabu, na za wana wa Amoni, na za Wafilisti, na za Amaleki, na za nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Basi Daudi akajipatia jina, alipokuwa akirudi, aliwaua Waedomi elfu kumi na nne katika bonde la chumvi. Akaweka askari wenye kulinda ngome katika Edomu; katikati ya Edomu yote akaweka ngome, na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi ushindi kila kokote alikokwenda. Daudi akatawala juu ya Israeli wote; naye Daudi akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. Huyo Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa majeshi; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, mwekaji kumbukumbu; na Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi wakawa makuhani.