Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 4

4
Israeli hajamrudia Mwenyezi Mungu
1Sikilizeni neno hili, ninyi ng’ombe wa Bashani
mlioko juu ya Mlima Samaria,
ninyi wanawake mnaowadhulumu maskini,
na kuwagandamiza wahitaji,
na kuwaambia wanaume wenu,
“Tuleteeni vinywaji!”
2Bwana Mungu Mwenyezi ameapa kwa utakatifu wake:
“Hakika wakati utakuja
mtakapochukuliwa na kulabu,
na wanaosalia kwa ndoana za samaki.
3Nanyi mtaenda moja kwa moja
kupitia mahali palipobomolewa kwenye ukuta,
nanyi mtatupwa nje kuelekea Harmoni,”
asema Mwenyezi Mungu.
4“Nendeni Betheli mkatende dhambi;
nendeni Gilgali mkazidi kutenda dhambi.
Leteni dhabihu zenu kila asubuhi,
zaka zenu kila mwaka wa tatu.
5Mchome mkate uliotiwa chachu kama sadaka ya shukrani,
jisifuni kuhusu sadaka zenu za hiari:
jigambeni kwa ajili ya sadaka hizo, enyi Waisraeli,
kwa kuwa hili ndilo mnalopenda kulitenda,”
asema Bwana Mungu Mwenyezi.
6“Niliwapa njaa kwenye kila mji,
na ukosefu wa chakula katika kila mji,
hata hivyo bado hamjanirudia mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
7“Pia niliwazuilia ninyi mvua miezi mitatu
kabla ya kufikia mavuno.
Nilinyesha mvua kwenye mji mmoja,
lakini niliizuia mvua isinyeshe mji mwingine.
Shamba moja lilipata mvua,
na lingine halikupata, nalo likakauka.
8Watu walitangatanga mji hata mji kutafuta maji,
lakini hawakupata ya kuwatosha kunywa,
hata hivyo hamjanirudia mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
9“Mara nyingi nilizipiga bustani zenu na mashamba ya mizabibu,
niliyapiga kwa kutu na ukungu.
Nzige walitafuna tini zenu na miti ya mizeituni,
hata hivyo hamjanirudia mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
10“Niliwapelekea tauni miongoni mwenu
kama nilivyofanya kule Misri.
Niliwaua vijana wenu wa kiume kwa upanga,
na nikawachukua farasi wenu.
Nilijaza pua zenu kwa uvundo kutoka kambi zenu,
hata hivyo hamjanirudia mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
11“Niliwaangamiza baadhi yenu kama
nilivyoangamiza Sodoma na Gomora.
Mlikuwa kama kijiti kiwakacho kilichonyakuliwa motoni,
hata hivyo hamjanirudia,”
asema Mwenyezi Mungu.
12“Kwa hiyo hili ndilo nitakalowafanyia, Israeli,
na kwa sababu nitawafanyia hili,
jiandaeni kukutana na Mungu wenu, ee Israeli.”
13Yeye ambaye hufanya milima, anaumba upepo,
na kufunua mawazo yake kwa mwanadamu,
yeye ageuzaye asubuhi kuwa giza,
na kukanyaga mahali pa juu pa nchi:
Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni
ndilo jina lake.

Iliyochaguliwa sasa

Amosi 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia