Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 9:1-19

Danieli 9:1-19 NENO

Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario mwana wa Ahasuero (mzaliwa wa Umedi), ambaye alifanywa mtawala wa ufalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, mimi Danieli nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu lililopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini. Kwa hiyo nikamgeukia Mwenyezi Mungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, na kuvaa gunia na kujipaka majivu. Nikamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, na kutubu: “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake, tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi. “Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: watu wa Yuda, na wakaaji wa Yerusalemu, na Waisraeli wote, walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu tulikosa uaminifu kwako. Ee Mwenyezi Mungu, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake. Hatukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuzishika sheria alizotupatia kupitia kwa watumishi wake, manabii. Israeli wote wamekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii. “Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Torati ya Musa, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu, kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka kwa Yerusalemu. Kama vile ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa kuacha kutenda dhambi na kuisikiliza kweli yake. Mwenyezi Mungu hakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ni mwenye haki katika kila afanyalo; lakini hata hivyo, hatujamtii. “Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu, na kujifanyia Jina linalodumu hadi leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya. Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako kwa Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka. “Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua za mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako angalia kwa huruma ukiwa wa mahali pako patakatifu. Ee Mungu, tega sikio, ukasikie; fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.”