Kutoka 25:1-9
Kutoka 25:1-9 NENO
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli waniletee sadaka. Utapokea sadaka kwa niaba yangu kutoka kwa kila mtu ambaye moyo wake wapenda kutoa. “Hizi ndizo sadaka utakazozipokea kutoka kwao: “dhahabu, fedha na shaba; nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu, pamoja na kitani safi; singa za mbuzi; ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita; mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezo kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri; na vito vya shohamu na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kizibau na kile kifuko cha kifuani. “Kisha uwaamuru wanitengenezee mahali patakatifu, nami nitakaa miongoni mwao. Tengeneza Maskani hii na vyombo vyake vyote sawasawa na kielelezo nitakachokuonesha.